Jeshi la DRC lasema ndege ya mizigo haijulikani ilipo huku waasi wakijidai kutungua ndege ya kivita

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 24, 2026

KINSHASA - Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) limesema kuwa limepoteza mawasiliano na ndege ya kijeshi ya mizigo, hivi sasa mahali ilipo ndege hiyo na wafanyakazi wake bado hakujulikani, wakati huo huo jeshi la waasi wamejidai kuwa limetungua ndege ya kivita ya serikali katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo linalokabiliwa na migogoro.

Msemaji wa upande wa jeshi la serikali Sylvain Ekenge, amesema katika taarifa ya jana Jumatatu kwamba jeshi la anga limepoteza mawasiliano na ndege nyepesi ya mizigo aina ya Cessna 208 iliyokuwa ikisafiri kati ya Beni katika Jimbo la Kivu Kaskazini na Kalemie katika Jimbo la Tanganyika.

Upande wa Jeshi umehusisha kupotea kwa mawasiliano hayo na hali mbaya ya hewa, lakini umesema ndege hiyo bado haijajulikana ilipo na hatima ya wafanyakazi wake haijulikani. Taarifa yake imesema shughuli za kutafuta ndege hiyo zinaendelea. Hata hivyo haikutoa maelezo zaidi kuhusu idadi ya watu waliokuwemo ndani ya ndege hiyo au mahali pa mwisho panapojulikana ambako ndege hiyo ilikuwa.

Habari hiyo ilitolewa siku moja baada ya kundi la Mstari Mbele wa Kujenga Upya Nchi (Front for the Refoundation of the Nation, FRN), vuguvugu la waasi la kisiasa na kijeshi linaloongozwa na Rais wa zamani wa DRC, Joseph Kabila, lilijidai kuwa limetungua ndege ya kivita ya serikali karibu na Minembwe, katika Jimbo la Kivu Kusini.

Minembwe iko kwenye njia kati ya majimbo ya Kivu Kaskazini na Tanganyika.

Taarifa ya upande wa jeshi haikujibu moja kwa moja madai hayo ya waasi, wala haikufafanua kama ndege hiyo ya mizigo ambayo haijulikani iliko ndiyo hiyohiyo ambayo kundi la FRN linadai kuitungua.

Maendeleo hayo ya hali ya mambo yametokea wakati mapigano mapya yanapamba moto tena katika eneo la mashariki mwa DRC, hasa katika Jimbo la Kivu Kusini, ambapo vikosi vya serikali na makundi washirika vinapambana na waasi wa FRN, ingawa juhudi za kikanda na kimataifa zinazoendelea zinahimiza upatanishi wa kusimamisha mapigano.Habari zilizotolewa hivi karibuni zimesema kuwa, mapigano yameripotiwa kufanyika katika maeneo ya nyanda za juu za Minembwe na sehemu nyingine za Kivu Kusini, hali ambayo inazua wasiwasi juu ya usalama wa raia na kusababisha watu wengi zaidi kukimbia makazi yao katika eneo hilo lililoathiriwa na migogoro.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha