Lugha Nyingine
Wanafunzi 30 wa kike wa DRC wapewa ufadhili wa masomo wa Mulan kutoka China

Balozi wa China nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Zhao Bin, akikabidhi vyeti na ufadhili wa masomo kwa wawakilishi wa wanufaika mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), tarehe 18 Novemba 2026. (Xinhua/Si Yuan)
KINSHASA – Wanafunzi wa kike jumla ya 30 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamepewa ufadhili wa masomo wa Mulan kwenye hafla iliyoandaliwa Jumatano wiki hii mjini Kinshasa na Ubalozi wa China, na kufikia mara ya tano ya mpango huo unaolenga kuunga mkono elimu na uwezeshaji wa wanawake katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Balozi wa China nchini DRC, Zhao Bin, Blaise Mbenga Aundu, mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu ya DRC; Jean-Marie Kayembe Ntumba, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kinshasa; pamoja na wanufaika wa ufadhili huo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Zhao amethibitisha tena dhamira ya China katika kuunga mkono elimu na maendeleo ya wanawake nchini DRC, huku akisisitiza kuzidisha ushirikiano wa pande mbili katika elimu ya juu, mafunzo ya ufundi, na mawasiliano ya kitamaduni kati ya watu.
Amewahimiza wanufaika hao kujifunza kutoka moyo wa Mulan, ambaye ni alama ya ushujaa na ustahimilivu wa mambo magumu katika utamaduni wa China, na kutumia maarifa pamoja na ujuzi wao kuchangia katika maendeleo ya nchi yao, na kuimarisha urafiki kati ya watu wa China na DRC.
Kwa upande wake, Mbenga Aundu amesema kuwa ufadhili huo wa masomo wa Mulan unaonesha umuhimu ambao nchi zote mbili zinaweka katika uendelezaji wa vipaji na uwezeshaji wa wanawake, huku pia ukisaidia kuendeleza ushirikiano wa kielimu kati ya China na DRC.
Ufadhili huo wa masomo wa Mulan, ambao ulianzishwa mwaka 2022 na Ubalozi wa China nchini DRC, umeshanufaisha wanafunzi wa kike zaidi ya 130 wa DRC, ukiwasaidia kuendelea na masomo yao na kufikia matarajio yao binafsi na ya kitaaluma.

Blaise Mbenga Aundu, mwakilishi wa Wizara ya Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), akizungumza kwenye hafla ya utoaji wa ufadhili wa masomo jijini Kinshasa, DRC, tarehe 18 Novemba 2026. (Xinhua/Si Yuan)

Maonesho ya picha ya China na Afrika yazidisha urafiki na uhusiano wa kiutamaduni

Maua mabichi yaliyokatwa ya Kenya yang’ara kwenye soko la China

Maonyesho ya urukaji wa ndege yafanyika Changchun kuadhimisha kuanzishwa kwa Jeshi la Anga la China

Shughuli ya Siku ya Meli ya "Xuelong 2" ya China kufunguliwa kwa umma yafanyika Hainan
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma