Iran yakataa madai ya fidia kutoka kwa Nchi za Ghuba

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 16, 2026

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, akizungumza kwenye mkutano wa wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Novemba 15, 2026. (Xinhua/Shadati)

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, akizungumza kwenye mkutano wa wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Novemba 15, 2026. (Xinhua/Shadati)

TEHRAN - Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amekataa madai ya Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC) kwamba Iran inapaswa kutoa fidia kwa uharibifu, hasara, na majeraha yaliyosababishwa na mashambulizi yake dhidi ya kambi na mali za Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Baghaei ametoa kauli hizo jana Jumapili kwenye mkutano wa wiki na waandishi wa habari, akijibu kauli dhidi ya Iran zilizotolewa na Katibu Mkuu wa GCC, Jasem Mohamed Albudaiwi, kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Ijumaa, kilichoitishwa kwa ombi la Bahrain.

Albudaiwi alisema kuwa tangu tarehe 28 Februari, Iran imerusha makombora na droni zaidi 7,000 dhidi ya nchi za Ghuba, na kwamba GCC inaitwika Iran wajibu kamili kwa mashambulizi hayo na matokeo yake.

Aliainisha madai ya GCC mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikiwemo "kuitaka Iran kutoa fidia kamili kwa uharibifu uliotokana na mashambulizi yake hayo, kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Azimio namba 61/1 la Baraza la Haki za Binadamu."

Akijibu madai hayo Baghaei amesema kuwa nchi za eneo hilo ambazo "zilishiriki kikamilifu katika uchokozi wa kijeshi" dhidi ya Iran na kuruhusu maeneo yao kutumiwa na "wachokozi" haziwezi kudai fidia.

Msemaji huyo wa Iran amesema kuna "ushahidi dhahiri" kwamba hasara na uharibifu kwa upande wa Iran ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja wakati wa vita hivyo vya siku 40, vilisababishwa na baadhi ya nchi katika kanda hiyo.

Amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Azimio la 3314 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, "nchi yoyote iliyoshiriki ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika uchokozi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, inachukuliwa kuwa mshirika wa wachokozi hao na inawajibika kwa uhalifu uliofanywa."

Amesema Iran ni upande unaodai fidia na kwamba tayari imekamilisha nyaraka zinazohitajika katika suala hilo.

Baghaei amesisitiza tena kwamba hatua za Iran za kujilinda "zilikuwa za kujihami na zililenga tu kambi za kijeshi na rasilimali za kijeshi za Marekani ambazo zilitumika kuanzisha mashambulizi" dhidi ya Iran. Akisisitiza kuwa Iran haikuchukua hatua yoyote dhidi ya mamlaka ya ardhi ya nchi hizo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, akizungumza kwenye mkutano wa wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Novemba 15, 2026. (Xinhua/Shadati)

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, akizungumza kwenye mkutano wa wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Novemba 15, 2026. (Xinhua/Shadati)

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha