Lugha Nyingine
Ujumbe wa China watembelea Ethiopia kwa ajili ya ushirikiano wa karibu zaidi katika tiba ya jadi

Picha hii iliyopigwa tarehe 11 Novemba 2026 ikionesha Taasisi ya Utafiti ya Armauer Hansen (AHRI) mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia. (Xinhua/Geng Xinning)
ADDIS ABABA - Ujumbe wa ngazi ya juu wa Tiba ya Jadi ya Kichina (TCM) umetembelea Taasisi ya Utafiti ya Armauer Hansen (AHRI) mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, jana Jumatano ili kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika utafiti na maendeleo ya tiba ya jadi.
Ujumbe huo, ukiongozwa na Gu Zhishan, profesa wa Chuo Kikuu cha Tiba ya Jadi ya Kichina cha Anhui, ulijadiliana na maafisa wa taasisi hiyo juu ya namna TCM inavyoweza kusaidia kukinga na kudhibiti magonjwa mbalimbali kwa kutumia mbinu za tiba zenye gharama nafuu za mazoezi ya viungo (physical therapies) na dawa za mitishamba.
Gu amesema kuwa TCM inalenga kuleta uwiano na mapatano kati ya mwili wa binadamu na mazingira ya asili, badala ya kutibu ugonjwa mmoja, na inatoa ahueni kwa aina mbalimbali za maradhi.
"Tunapenda kutumia fursa hii kuchangia nanyi maarifa yetu juu ya TCM, ambayo inajumuisha huduma za kinga na tiba za asili," amesema Gu, huku akisisitiza kuwa wataalamu wa TCM wana nia ya kuchangia maarifa yao na wenzao wa Ethiopia.
Messay Woldemariam, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa AHRI, amesema kuwa Ethiopia inajaribu kufungamanisha tiba za jadi na zile za kisasa, akibainisha kuwa uzoefu na maarifa ya muda mrefu ya China katika tiba ya jadi vitakuwa na umuhimu mkubwa katika kuendeleza tiba za jadi nchini Ethiopia.
"China inaweza kusaidia kuendeleza tiba za jadi za Ethiopia na kupanua matumizi ya dawa za mitishamba katika kutibu magonjwa mbalimbali. Kuna dawa za mitishamba takribani 600 zilizosajiliwa nchini Ethiopia, na tunataka uungaji mkono wa China ili kuziendeleza kuwa bidhaa mpya," amesema.
Pia ametoa wito wa ushirikiano wa karibu zaidi katika maendeleo ya bidhaa na uwekaji vigezo vyao, utafiti wa pamoja, ujengaji uwezo, ujengaji mitandao ya kisayansi, na ushirikiano kati ya taasisi za pande hizo mbili.
Ujumbe huo pia ulitembelea Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA) siku ya Jumanne, ambapo Gu aliwaelezea maafisa ya kamisheni hiyo juu ya nafasi ya TCM katika kuhimiza mapatano kati ya binadamu na mazingira ya asili, pamoja na mbinu zake katika kukinga na kutibu magonjwa.

Ujumbe wa ngazi ya juu wa Tiba ya Jadi ya Kichina (TCM) ukiongozwa na Gu Zhishan (wa pili kushoto, mbele), profesa wa Chuo Kikuu cha Tiba ya Jadi ya Kichina cha Anhui, ukifanya majadiliano na maafisa wa Taasisi ya Utafiti ya Armauer Hansen (AHRI) mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, Novemba 11, 2026. (Xinhua/Geng Xinning)

Messay Woldemariam (wa pili, kulia), naibu mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Armauer Hansen (AHRI), akihudhuria majadiliano na ujumbe wa ngazi ya juu wa Tiba ya Jadi ya Kichina (TCM) katika taasisi hiyo mjini Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, Novemba 11, 2026. (Xinhua/Geng Xinning)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



