Lugha Nyingine
China yakabidhi mabaki ya wanajeshi wa kikosi cha anga cha Marekani yaliyopatikana kwenye Njia ya Hump ya WWII

Nyaraka inayothibitisha kukabidhiwa kwa mabaki ya wanajeshi wa kikosi cha anga cha Marekani yaliyopatikana kwenye Njia ya Hump ikisainiwa, huku wawakilishi wa China na Marekani wakishuhudia, kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika Chengdu, Mkoa wa Sichuan, kusini-magharibi mwa China, Novemba 10, 2026. (Xinhua/Xu Bingjie)
CHENGDU – Wanajeshi wa gwaride la heshima wa China walisonga mbele, wakishika sanduku lenye mabaki ya binadamu. Wanajeshi wa gwaride la heshima wa Marekani walisogea mbele kulipokea na kuliwekea kwa uangalifu bendera ya taifa la Marekani juu yake.
Sanduku hilo lilikuwa na vipande nane vya mifupa vilivyopatikana kwenye barafu iliyo katika mwinuko wa mita zaidi 5,000 juu ya usawa wa bahari. Mabaki hayo, yanayoaminika kuwa ya wanajeshi wa kikosi cha anga cha Marekani waliopotea kwenye Njia ya Hump wakati wa Vita vya Pili vya Dunia (WWII), yalikuwa yamelala milimani kwa miaka zaidi ya 80.
Kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika Chengdu, Mkoa wa Sichuan kusini-magharibi mwa China, jana Jumanne, He Jiang, Mkurugenzi wa Nyaraka za Kumbukumbu za Jeshi la Ukombozi wa Umma la China, na Kapteni wa Jeshi la Majini la Marekani, Colin Alexander Eliot—mtaalamu wa uchunguzi wa kisayansi kutoka Shirika la Marekani la Utafutaji wa Watu Wasiojulikana Waliko Vitani (DPAA)—walitia saini nyaraka inayothibitisha makabidhiano hayo, huku wawakilishi wa China na Marekani wakishuhudia.
Mabaki hayo yalipatikana kwenye maeneo yaliyo kwenye Njia ya Hump, ambayo ilianzishwa baada ya vikosi vya Japan kuiteka Myanmar mwaka 1942, ambapo Wajapani walikata barabara ya Yunnan-Myanmar—njia kuu ya mwisho ya China ya kusafirisha bidhaa kwenye nchi kavu inayounganisha ndani na nje ya China.
Ushoroba huo wa anga, unaoanzia jimbo la Assam kaskazini-mashariki mwa India hadi Kunming kusini-magharibi mwa China na kupita juu ya milima ya Himalaya, ilikuwa njia muhimu sana ya kusafirisha mahitaji muhimu kwa washirika waliounga mkono mapambano ya China dhidi ya uvamizi wa Japan kuanzia mwaka 1942 hadi 1945.
Wafanyakazi wa ndege wa China na Marekani zaidi ya 1,000 walipoteza maisha kwenye njia hiyo. Kutokana na milima mirefu na barafu kufanya shughuli za utafutaji kuwa ngumu sana, mabaki ya wengi wao hayajawahi kupatikana.
Vipande hivyo vilivyokabidhiwa jana Jumanne vilipatikana kwa juhudi za timu ya utafutaji iliyoandaliwa na Jumba la Makumbusho la Jianchuan, jumba linaloendeshwa na sekta binafsi katika mkoa wa Sichuan—wakati wa utafutaji kwenye barafu za Nyingchi, katika Mkoa Unaojiendesha wa Xizang, kusini-magharibi mwa China.
China na Marekani zimekuwa zikishirikiana katika kutafuta wanajeshi wa Marekani waliopotea wakati wa Vita vya Pili vya Dunia tangu miaka ya 1970. Mamlaka za China pamoja na makundi ya kiraia wamechangia katika juhudi hizo.
"Mabaki haya yanabeba ushuhuda wa vita dhidi ya ufashisti na yanabeba historia ya watu wa China na Marekani wakipambana dhidi ya uchokozi pamoja," amesema Fan Jianchuan, msimamizi wa Jumba la Makumbusho ya Jianchuan. "Pia yanatukumbusha kuimarisha ushirikiano na kutoa michango mipya kwenye amani duniani."
Akizungumza katika hafla hiyo, Eliot amezungumzia kuchangia historia ya wakati wa vita ambayo mabaki hayo yanaiwakilisha.
"Mabaki yaliyo mbele yetu yanawakilisha wakati muhimu wa kihistoria wakati Wamarekani, wakisukumwa na wajibu wa kulinda dhidi ya uchokozi, walisimama bega kwa bega na watu wa China kupambana na tishio linalofanana," amesema.

Wanajeshi wa Gwaride la Heshima wa China wakikabidhi sanduku lenye mabaki ya wanajeshi wa kikosi cha anga cha Marekani yaliyopatikana kwenye Njia ya Hump kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika Chengdu, Mkoa wa Sichuan, kusini-magharibi mwa China, Novemba 10, 2026. (Xinhua/Xu Bingjie)

Wanajeshi wa Gwaride la Heshima la Marekani wakipokea sanduku lenye mabaki ya wanajeshi wa kikosi cha anga cha Marekani yaliyopatikana kwenye Njia ya Hump kwenye hafla ya makabidhiano iliyofanyika Chengdu, Mkoa wa Sichuan, kusini-magharibi mwa China, Novemba 10, 2026. (Xinhua/Xu Bingjie)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



