Wataalamu wa China watoa mafunzo kwa wataalamu wa vyombo vya habari wa Tanzania katika matumizi ya AI

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Novemba 03, 2026

Wataalamu wa vyombo vya habari wa Tanzania wakihudhuria programu ya mafunzo ya vyombo vya habari katika AI kati ya China na Afrika jijini Dar es Salaam, Tanzania, Novemba 1, 2026. (Xinhua/Emmanuel Herman)

DAR ES SALAAM – Mamlaka ya Kitaifa ya Redio na Televisheni ya China (NRTA) imefanya programu ya mafunzo ya siku mbili kwa wataalamu wa vyombo vya habari wa Tanzania ili kuimarisha ujuzi wa kidijitali, kuboresha uzalishaji maudhui, na kutafuta uwezekano wa fursa mpya za biashara.

Programu hiyo, iliyopewa jina la "Mafunzo ya Vyombo vya Habari katika AI kati ya China na Afrika," imefanyika kuanzia Jumapili jijini Dar es Salaam, Tanzania, ikiwaleta pamoja wataalamu wapatao 30 kutoka idara za uzalishaji maudhui ya vyombo vya habari, uandaaji vipindi, ubunifu, mambo ya kidijitali, na kiufundi.

Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian amesema AI inabadilisha kwa kasi tasnia ya vyombo vya habari kupitia programu kama vile tafsiri otomatiki, usomaji wa kuthibitisha usahihi, utengenezaji wa maandishi hadi video, watangazaji wa kidijitali na studio pepe.

Amesema China imedhamiria kuzisaidia nchi za Afrika kuimarisha uwezo wa kidijitali na kuziba pengo la kidijitali, akisisitiza kwamba maendeleo ya AI yanapaswa kuwa jumuishi na yenye kunufaisha wote.

Yang Yong, naibu mkurugenzi mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya NRTA, amesema mpango huo unalenga kuimarisha uwezo wa kiufundi, kukuza vipaji na kuhimiza uelezaji simulizi wa pamoja kati ya China na Afrika.

“Mafunzo haya yanaweka mkazo katika matumizi ya kivitendo ya AI zalishi katika uzalishaji maudhui wa vyombo vya habari, utangazaji wa utalii, uelezaji simulizi za kitamaduni, matangazo ya kibiashara ya televisheni na kuyafanya maudhui kuwa ya kibiashara,” amesema, akiongeza kuwa mafunzo hayo yanatumia mbinu ya "kufunza-mkufunzi" ili kukuza wakufunzi wenyeji na kuleta ujuzi wa AI kwa wataalamu zaidi wa vyombo vya habari wa Afrika.

Sheba Kussaga, mkurugenzi wa maendeleo ya biashara katika Kampuni ya Vyombo vya Habari ya Clouds yenye makao yake makuu Tanzania, amesema mafunzo hayo yataongeza ufanisi, tija na uwezo wa kushindana wa wafanyakazi.

Mbarouk Khan, mtangazaji wa redio na mbunifu maudhui ya kidijitali aliyehudhuria mafunzo hayo, amesema ujuzi wa AI utamsaidia kuzalisha maudhui ya mitandao ya kijamii yenye ubora wa juu, kuboresha tija na uwezekano wa kuongeza mapato yake.

Ametoa wito wa kuwepo fursa zaidi za mafunzo ili kusaidia wataalamu vijana wa vyombo vya habari wa Tanzania kubadilika kuendana na teknolojia zinazoibuka.

Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, akizungumza kwenye programu ya mafunzo ya vyombo vya habari katika AI kati ya China na Afrika, jijini Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 1 Novemba 2026. (Xinhua/Emmanuel Herman)

Yang Yong (kulia), Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Mamlaka ya Kitaifa ya Redio na Televisheni ya China (NRTA), na Sheba Kussaga, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara katika Kampuni ya Vyombo vya Habari ya Clouds yenye makao yake nchini Tanzania, wakipiga picha wakiwa wameshikilia mkataba wa ushirikiano uliotiwa saini kwenye programu ya mafunzo ya vyombo vya habari katika AI kati ya China na Afrika, jijini Dar es Salaam, Tanzania, tarehe 1 Novemba 2026. (Xinhua/Emmanuel Herman)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha