Lugha Nyingine
Iran yaashiria kuufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz ndani ya siku 2 kama Marekani itatimiza matakwa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, akihudhuria mkutano wa wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, tarehe 2 Novemba 2026. (Xinhua/Shadati)
TEHRAN/WASHINGTON - Iran imeashiria kuwa inaweza kuufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz na kurejea kwenye mazungumzo ya kidiplomasia ndani ya siku mbili kama Marekani itatimiza matakwa yake.
Akizungumza kwenye mkutano wa wiki na waandishi wa habari jana Jumatatu, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema kwamba kama matakwa ya Iran yatatimizwa, uwezekano utakuwepo kurejesha usalama kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz na kuanza mchakato wa mazungumzo ndani ya muda mfupi. Amesisitiza kuwa yote hayo yanategemea uamuzi wa upande wa Marekani juu ya namna ya kuendelea kuhusiana na mustakabali wa mchakato huo.
Sambamba na tangazo hilo la wizara, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, alisema siku hiyo hiyo ya Jumatatu kuwa serikali yake imedhamiria kutatua changamoto kupitia mazungumzo, akibainisha kuwa Kiongozi Mkuu, Mojtaba Khamenei, ameipa serikali mamlaka fulani ya kutafuta suluhu za kidiplomasia.
Amesisitiza kuwa hakuna anayenufaika na vita, akiongeza kuwa "maadui" hawataweza kuifanya Iran kusalimu amri.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Seyed Abbas Araghchi, alisema mashauriano yanayowezeshwa na Qatar na Pakistan yamekuwa "mapana zaidi," yakihusisha ziara za mara kwa mara za wajumbe, mazungumzo kwa njia ya simu, na kutumiana ujumbe.
Akisisitiza tena utayari wa Iran kwa vyote diplomasia na ulinzi, Araghchi ameonya kuwa hatua yoyote ya kijeshi zaidi kutoka Washington itasababisha jibu "chungu na kali zaidi."
Jitihada hizi za kidiplomasia zinafanyika huku kukiwa na ishara zinazokanganya kutoka Washington juu ya hatua yake inayofuata dhidi ya Iran.
Inaripotiwa kuwa Tehran ilipokea barua Alhamisi wiki iliyopita kutoka kwa Makamu Rais wa Marekani, JD Vance—iliyotumwa kwa maelekezo ya Trump—ikitoa wito wa kurejea kwa mazungumzo ya amani. Iran imeyaelezea mabadiliko hayo katika msimamo wa Washington unaojionesha kupitia barua hiyo kuwa ni "ishara nzuri."
Hata hivyo, Rais wa Marekani, Donald Trump, juzi Jumapili alitishia tena kuanzisha upya hatua za kijeshi dhidi ya Iran "wakati fulani," akisema kwenye mkutano wa kampeni huko Iowa kwamba Washington hatimaye italazimika "kuwapa nyundo."
Pia jana Jumatatu, Rais Trump, alisema kuwa Tehran inataka kufikia makubaliano na Washington, na kwamba makubaliano hayo yanaweza kufikiwa.
Harakati hizi za kidiplomasia zinaambatana na maandalizi thabiti ya kijeshi na kupamba moto kwa hatari za kioperesheni katika eneo hilo.
Kamanda mmoja mwandamizi wa Iran alisema jana Jumatatu kuwa Wairani zaidi ya milioni 30 wako wanapata mafunzo ya kijeshi ili kulinda nchi iwapo itahitajika.
Uhamasishaji huo wa kijeshi unafuatia taarifa iliyotolewa Jumamosi na Kiongozi Mkuu wa Iran Mojtaba Khamenei akiwaagiza makamanda waandamizi wa jeshi kuhakikisha kuwa tishio lolote kutoka kwa "maadui," bila kujali asili au ukubwa wake, linakabiliwa na jibu la "haraka na thabiti," bila mipaka ya kijiografia.
Kwa upande wa Marekani, jarida la Wall Street limeripoti kuwa maafisa waandamizi wa jeshi la Marekani walimpa Trump taarifa Alhamisi wiki iliyopita juu ya machaguo mbalimbali yanayowezekana kuchukuliwa dhidi ya Iran. Inasemekana pia kuwa Marekani imezihimiza nchi kadhaa za Ghuba kujiandaa kwa uwezekano wa operesheni ya kijeshi—fupi lakini kali—dhidi ya Iran baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, akihudhuria mkutano wa wiki na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, tarehe 2 Novemba 2026. (Xinhua/Shadati)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



