Lugha Nyingine
Matokeo ya awali nchini Israel yaonesha kambi ya Netanyahu ikiongeza viti huku kukiwa hakuna mshindi wa moja kwa moja

Gadi Eisenkot (kushoto mbele), mkuu wa zamani wa jeshi la Israel na kiongozi wa chama cha mrengo wa kati cha Yashar, akipiga kura yake kwenye kituo cha kupigia kura huko Herzliya, katikati mwa Israel, Oktoba 27, 2026. (JINI kupitia Xinhua)
YERUSALEMU - Matokeo mapya ya awali ya kura za maoni kutoka kwenye vituo vya kupigia kura yanaonesha kambi ya mrengo wa kulia ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ikiongeza viti zaidi huku kura zikiendelea kuhesabiwa mapema leo Jumatano, ingawa hata hivyo, si kambi yake wala ile ya mpinzani wake mkuu, Gadi Eisenkot, iliyopata wingi wa viti bungeni kuweza kuunda serikali peke yake.
Vituo vitatu vikuu vya televisheni vimerekebisha makadirio yao ya kura za maoni wakati Tume Kuu ya Uchaguzi ya Israel ilipoanza kutoa matokeo ya awali ya kura zilizopigwa.
Kituo cha 'Channel 12' kimekadiria kuwa kambi ya Netanyahu itapata viti 52 na kambi ya Eisenkot viti 49, huku vyama vya Waarabu vikichukua viti 19 vilivyobaki katika bunge lenye jumla ya viti 120.
Kituo cha taifa cha televisheni cha Israel, Kan TV News na Channel 13 vimekadiria idadi sawa ya viti kati ya kambi hizo mbili pinzani, kila moja ikipata viti 51, wakati vyama vya Waarabu vikitarajiwa kupata viti 18.
Makadirio hayo yaliyorekebishwa yanaashiria badiliko kutoka matokeo ya awali ya kura za maoni yaliyotolewa jana Jumanne usiku, ambayo yalionesha kambi ya Eisenkot ikiwa na wingi kidogo dhidi ya kambi ya Netanyahu.
Hakuna kambi iliyofikia viti 61 vinavyohitajika ili kupata wingi kamili bungeni. Vyama vya Waarabu, ambavyo si sehemu ya kambi yoyote kati ya hizo mbili, vinaweza kuwa na nguvu ya kuamua mwelekeo wa kisiasa, ingawa Netanyahu na Eisenkot wote wamekataa uwezekano wa kuviingiza vyama hivyo kwenye serikali ya mseto.
Makadirio haya yasiyo ya mwisho yanaiacha Israel ikikabiliwa na uwezekano wa mazungumzo ya muda mrefu ya kuunda serikali ya mseto, huku zoezi rasmi la kuhesabu kura likiendelea.
Akihutubia wafuasi wake mapema leo Jumatano, Netanyahu amesema kuwa chama cha Likud kimeibuka kuwa chama kikubwa zaidi nchini Israel, na ameonya dhidi ya kuviingiza vyama vya Waarabu kwenye serikali yoyote ya mseto, akiielezea hatua hiyo kuwa ni "tishio" kwa Israel.
Aidha, amedokeza uwezekano wa kupamba moto zaidi mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati, akisema: "Israel inakabiliwa na fursa ya kipekee ya kihistoria pamoja na mshirika wetu (Rais wa Marekani Donald) Trump, ya kuondoa tishio la Iran."
Mapema leo, Eisenkot aliwasili kwenye makao makuu ya kampeni yake kukutana na wafuasi wake, akisema kuwa muungano unaotawala wa Netanyahu umepoteza imani ya umma na kwamba wapiga kura wamekataa muhula wake mwingine.
"Usiku wa leo, tumepata jibu. Umma umepigia kura mabadiliko," amesema Eisenkot.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



