Shajara ya Shenzhen, China siku ya pili: Maktaba na Sanaa vyabeba ushuhuda wa maendeleo ya kasi na usahihi bila kuacha mambo mazuri

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 21, 2026

Mandhari ya nje ya Jengo la Kaskazini la Maktaba ya Shenzhen, China. (People’s Daily Online)

Mandhari ya nje ya Jengo la Kaskazini la Maktaba ya Shenzhen, China. (People' s Daily Online)

Jana asubuhi Jumanne, siku yangu ya pili nikiwa katika Mji wa Shenzhen wa China, mji unaopiga hatua ya maendeleo kwa kasi ya ajabu lakini bado unatilia maanani sana kuhifadhi utulivu wa zamani, niliianza siku katika moyo wa mji huu. Safari yangu moja kwa moja ilikuwa kwenye jengo la maarifa, Maktaba ya Shenzhen, Upande wa Kaskazini, jengo ambalo linasimama kama alama ya usanifu wa kisasa ndani ya mazingira ya mjini yenye minara mirefu, barabara zenye magari mengi, na maisha yanayoendelea bila kukoma.

Jengo hili la Kaskazini la Maktaba ya Shenzhen lilifunguliwa kwa matumizi ya majaribio Septemba 28, 2023 na kufunguliwa rasmi Desemba 28 mwaka huo. Ni kundi la kwanza la miradi iliyokamilishwa ya "miundombinu mikubwa ya kitamaduni ya Shenzhen katika zama mpya".

Jengo hili lipo katika Wilaya ya Longhua, kituo cha jiografia na jiometri ya Shenzhen na mhimili mkuu wa maendeleo ya mji huu. Limejengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 72,000, likiwa na ghorofa 6 juu ya ardhi na ghorofa 3 chini ya ardhi. Limesanifiwa kuwa na uwezo wa kukusanya vitabu milioni 8 na viti 2,500 vya watu kuketi kujisomea kwa wakati mmoja.

Mara tu baada ya kufika karibu na eneo lilipo jengo hili nilijikuta ghafla nikisimama na kuduwaa huku nikibaki mdomo wazi. Uso wa jengo hili unaonekana kama “mchemraba wa maarifa” unaozunguka kidogo—uso wa mawe meusi yenye umbo la almasi ukiwa umeunganishwa na kuta za vioo zenye uwazi nusu. Limeunganishwa kwa barabara na mazingira yake ya mjini: liko karibu na Jumba la Sanaa la Shenzhen, vikichangia kutengeneza kituo cha utamaduni katikati ya Longhua, sehemu ambayo inaendelea kujengwa kwa kasi lakini bado inahifadhi nafasi za kijani.

Watu wakijisomea ndani ya Maktaba ya Shenzhen, China. (People’s Daily Online)

Watu wakijisomea ndani ya Maktaba ya Shenzhen, China. (People’s Daily Online)

Nilichovutiwa nacho zaidi ni teknolojia na mifumo ya roboti iliyofungwa ndani ya maktaba hii. Chini ya ardhi, katika tabaka tatu za chini zenye urefu wa zaidi ya mita ishirini na moja, kuna hifadhi ya vitabu yenye teknolojia za AI zaidi nchini China.

Ndani ya mfumo huo wa AI wa kuhifadhi, kupeleka na kurudisha vitabu kuna maelfu ya masanduku yenye vitabu milioni nne hivi. Unapotuma ombi la kuazima kitabu kupitia simu yako, mfumo wa AI unachagua njia bora zaidi. Mikono ya roboti huchukua sanduku, mikanda ya usafirishaji inasogea, na magari madogo yasiyo na dereva (AGV) yanachukua kitabu na kukiwasilisha kwenye dawati la huduma kwa dakika kumi tu bila kumhitaji mtu kujongea hata kidogo.

Nilichoshuhudia, ni kile ninachoweza kukieleza kuwa ni maisha ya mjini ya Shenzhen ambayo ni yenye kuhitaji teknolojia ya hali ya juu katika karibu kila jambo kuingia ndani ya maktaba: kasi, usahihi, na urahisi, lakini bado yanahifadhi utulivu wa kusoma na kutafakari.

Mfumo wa AI wa kuchukua, kupeleka na kurudisha vitabu ndani ya Maktaba ya Shenzhen, China. (People’s Daily Online)

Mfumo wa AI wa kuchukua, kupeleka na kurudisha vitabu ndani ya Maktaba ya Shenzhen, China. (People’s Daily Online)

Baadaye mchana nilielekea kaskazini mwa Shenzhen, hadi Jumuiya ya Guanlan Datian katika Wilaya ya Longhua. Mabadiliko yalikuwa kimyakimya lakini dhahiri sana. Minara mirefu ya majengo ikaanza kupungua, njia zenye miti na majengo ya chini ya kale yakaanza kuonekana, na hewa ikabadilika kidogo—sasa ikawa ni harufu ya wino, udongo, na majani.

Hapa nilikwenda kutembelea Kituo Asilia cha Picha za Kuchapwa cha Guanlan (Guanlan Printmaking Original Industrial Base) ambacho, ni maskani ya Chen Yanqiao, mwanzilishi wa vuguvugu la kukata na kuchonga magogo kutengeneza sanaa wa China. Usanifu wa eneo zima hili unachanganya nyumba za jadi za Hakka—nyumba za mstari, majumba ya mababu, visima vya zamani, mabwawa, na minara ya ulinzi—na majengo mapya ya karakana za picha za kuchapishwa.

Geti la kuingia ndani ya Kituo Asilia cha Picha za Kuchapwa cha Guanlan katika Eneo la Longhua, Shenzhen, China. (People’s Daily Online)

Geti la kuingia ndani ya Kituo Asilia cha Picha za Kuchapwa cha Guanlan katika Eneo la Longhua, Shenzhen, China. (People’s Daily Online)

Nilichoshuhudia hapa ni kwamba teknolojia ya kisasa haijidhihirishi kwa roboti nyingi kama ilivyo kwenye maktaba, lakini mchanganyiko wa maisha ya jadi na mji wa kisasa unaonekana dhahiri. Kwa mfano, karakana za kuchapisha picha zinatumia zana za zamani pamoja na vifaa vipya, na kijiji cha wasanii wa kimataifa kimebadilisha nyumba za zamani za Hakka kuwa studio za kisasa bila kufuta taswira zake za asili.

Cha kuvutia zaidi hapa, miti mikubwa, mito midogo, na vilima vya karibu vinafanya eneo hili liwe kama oasisi ndani ya Longhua yenye maendeleo. Nilitembea kati ya yadi, nikasikia sauti za vyombo vya uchapishaji, na nikaona jinsi mji wa Shenzhen unavyoruhusu desturi ya zamani kuishi pamoja na maendeleo yake.

Uchapishaji huu kwenye karakana nilizotembelea hapa unaendelea kutoa kazi, sanaa, na utamaduni huku ukiwa umezungukwa na barabara mpya, majengo ya biashara, na maisha yenye kasi ya mjini.

Nilirudi chumbani kwangu hotelini jioni nikiwa nimebeba picha mbili katika akili yangu: maktaba yenye roboti, mikono ya roboti, na magari madogo yasiyo na dereva yanayofanya vitabu kufika haraka ndani ya jengo lenye usanifu wa kisasa, na Guanlan yenye nyumba za Hakka, wino, na karakana za zamani zikiishi ndani ya mazingira ya mjini.

Shenzhen haijafuta maisha ya jadi; imeunganisha teknolojia ya roboti na usanifu wa kisasa na desturi za zamani ili vyote viwe na nafasi. Katika siku hii nilihisi shukrani kwa mji huu unaojua namna ya kukimbia mbele kwa kasi na usahihi bila kuacha nyuma kile kilichokuwa kizuri.

Waandishi wa habari wa People’s Daily Online wakifurahia picha pamoja na msanii kutoka Ujerumani kwenye moja ya karakana ndani ya Kituo Asilia cha Picha za Kuchapwa cha Guanlan katika Eneo la Longhua, Shenzhen, China. (People’s Daily Online)

Waandishi wa habari wa People’s Daily Online wakifurahia picha pamoja na msanii kutoka Ujerumani kwenye moja ya karakana ndani ya Kituo Asilia cha Picha za Kuchapwa cha Guanlan katika Eneo la Longhua, Shenzhen, China. (People’s Daily Online)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha