Lugha Nyingine
Shajara ya Shenzhen, China katika siku ya kwanza: Hifadhi ya Mazingira ya Asili ya Mikoko ya Futian, Mapafu ya Kijani Katikati ya Mji

Muongozaji akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu Hifadhi ya Kitaifa ya Mazingira ya Asili ya Guangdong Neilingding Futian mjini Shenzhen, mkoani Guangdong, China (People’s Daily Online)
Jana Jumatatu Oktoba 19 hatimaye nimeweza kuingia ndani ya Hifadhi ya Kitaifa ya Mazingira ya Asili ya Guangdong Neilingding Futian ambayo ndani yake pamoja na mambo mengine makubwa ya kiikolojia kuna Hifadhi ya Mazingira ya Asili ya Mikoko ya Futian mjini Shenzhen, mkoani Guangdong, China.
Hifadhi hii, ambayo kwangu mimi naipa jina la mapafu ya kijani katikati mwa mji wa kisasa, iko kaskazini mashariki mwa Ghuba ya Shenzhen, kutoka mdomo wa Mto Xinzhou katika upande wa mashariki mwa Bustani ya Ghuba ya Shenzhen hadi eneo la upande wa nje wa bahari lililopo nje ya matope na mdomo wa sehemu ya kusini ya Shenzhen, na hadi Barabara Kuu ya Guangshen kaskazini. Ina urefu wa takriban kilomita 6 kando ya ukanda wa pwani.
Sehemu ya mikoko ya Futian ya hifadhi hii iko kwenye pwani ya kaskazini-mashariki ya Ghuba ya Shenzhen, karibu sana na majengo marefu na barabara za katikati ya mji. Ina eneo la takriban hekta 367.64, na ni hifadhi pekee ya kiwango cha kitaifa nchini China iliyoko ndani kabisa ya mji mkubwa.
Mwaka 2020, mikoko hii ya Futian ilijumuishwa kwenye orodha ya kitaifa ya China ya maeneo oevu muhimu, na mwaka 2022, ilijumuishwa kwenye orodha ya kimataifa ya maeneo oevu muhimu. Kuna spishi 353 za mimea ya mishipa maalum katika msitu huu. Miongoni mwao, mikoko inachukua eneo la hekta takriban 100, ikiwa na spishi 20 za mimea ya mikoko ya familia 9, na spishi 7 za mimea halisi ya mikoko inayokua kiasili ndani ya msitu huu Pamoja na Kisiwa cha Neilingding kilicho ng’ambo ya maji. Hifadhi hiyo nzima ina eneo la hekta karibu 921.
Siku hii ya kutembelea hifadhi nilikuwa nimeisubiri kwa hamu na kwa muda mrefu, nikisoma kuhusu mahali hapa na kuhisi hamu ya kuona kwa macho yangu namna mazingira ya asili yanaweza kuishi kwa mapatano pamoja na binadamu na maendeleo ya kisasa.
Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bao'an wa Shezhen kutokea Beijing, mji mkuu wa China mapema mchana siku hiyo sikuweza kusubiri sana kabla ya kupanda basi maalum kuelekea hotelini na muda mfupi tu baadaye kuelekea kwenye hifadhi hii. Nikivuka barabara na minara mirefu ya majengo hadi kufika kwenye geti la hifadhi hii. Nje kulikuwa na kelele za magari na watu, lakini mara tu nilipoingia ndani, dunia ilibadilika kabisa
Kelele za ndege na insekta zilishika kasi. Miruzi ya viumbe mbalimbali wakiimba kwa kupokezana, ilipamba anga yote na kuifanya hifadhi iwe kama bustani ya peponi ambayo muda wote imejaa pilika zilizojaa maisha yasiyo na kikomo, lakini pia sauti za kuweza kukufanya uhisi kwamba kifo pengine hakijaumbiwa binadamu. Ni kama unakuwa uko ndani ya mfungo wa peponi vile ambao hutaki kabisa uishe.

Hifadhi ya Kitaifa ya Mazingira ya Asili ya Guangdong Neilingding Futian mjini Shenzhen, mkoani Guangdong, China (People's Daily Online)
Hewa ilikuwa na harufu laini ya chumvi kutoka eneo la mawimbi, mchanganyiko wa matope, majani ya mikoko, na hewa safi ya bahari. Mikoko minene—ya spishi dazeni kadhaa kutoka familia mbalimbali—imeunda kizuizi hai cha mizizi na majani ya kijani. Mizizi hiyo ambayo imetoka nje mithili ya mikono ya mtu, imeshikilia udongo na kutoa makazi kwa viumbe wadogo.
Nikiwa hapo, nikiangalia Hifadhi ya Mai Po ya Hong Kong upande wa pili wa ghuba, nilihisi jinsi ukanda huu mwembamba wa ardhi oevu unavyounganisha sehemu mbili kuwa mfumo-ikolojia mmoja wa maisha. Maji ya ghuba yalikuwa tulivu leo, yakiangaza jua la jioni, na mbali kidogo niliweza kuona mawingu mepesi yakielea juu ya milima ya Hong Kong.

Muongozaji akitoa maelezo kwa waandishi wa habari kuhusu Hifadhi ya Kitaifa ya Mazingira ya Asili ya Guangdong Neilingding Futian mjini Shenzhen, mkoani Guangdong, China (People’s Daily Online)
Nilitembea kwenye njia ya mbao iliyojengwa kwa umakini na ustadi mkubwa ili isisumbue mazingira. Kila hatua nilikuwa nikiangalia chini, nikiogopa kukanyaga kitu chochote cha thamani. Zaidi ya mikoko kulikuwa na maeneo ya matope na mabwawa ya samaki yaliyosimamiwa kwa umakini. Mabwawa haya si ya kawaida; yamebadilishwa kutoka eneo la ufugaji wa samaki wa zamani kuwa makazi bora kwa ndege.
Kuhama hama kwa ndege kwa majira ya mpukutiko kumeelezwa na muongozaji wa kundi la waandishi wa habari wa kigeni na wa China wa kuitazama Shenzhen kutoka People's Daily Online kuwa kumeanza mapema. Niliweza kuwaona ndege wa pwani na makundi ya kwanza ya spoonbill wenye uso mweusi wakichungulia madimbwi madogo ya maji kwa midomo yao maalum yenye umbo la kijiko. Walikuwa wakitafuta chakula kwa utulivu, wakitembea polepole na kutikisa midomo yao majini.

Hifadhi ya Kitaifa ya Mazingira ya Asili ya Guangdong Neilingding Futian mjini Shenzhen, mkoani Guangdong, China (People’s Daily Online)
Data ya ufuatiliaji inaonesha kuwa Ghuba ya Shenzhen, pamoja na upande wa Hong Kong, ilirekodi spoonbill 341 wenye uso mweusi katika sensa ya kimataifa ya 2026—takriban asilimia 4.4 ya idadi yote duniani. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, karibu ndege 100,000 wa majini wa kuhama hama hufika katika kituo hiki kila mwaka kwenye njia ya uhamaji ya Asia Mashariki–Australasia. Zaidi ya spishi 270 za ndege zimeandikishwa hapa, pamoja na spishi nyingi zinazolindwa kitaifa. Nimeweza pia kuona herons, cormorants, na sandpipers mbalimbali. Kila mara ndege alipopaa, moyo wangu uliruka pamoja naye.
Kilichonivutia zaidi ni jinsi mji huu ulivyochagua kwa makusudi kulinda mahali hapa. Miaka ya 1990, barabara iliyokuwa imepangwa ya Binhai Avenue ilihamishwa mita 260 kaskazini ili kuepuka eneo la msingi. Ulikuwa ni uamuzi mgumu kwa sababu mji ulikuwa unakua haraka sana, lakini wapanga mji walichagua mazingira ya asili.
Ukuta wa kuwalinda ndege na kelele wa mita 500 ulijengwa ili kupunguza sauti za magari, majengo ya karibu yalizuiliwa urefu ili yasivuruge ndege, uvuvi ulipigwa marufuku katika ghuba yote tangu 2014, na viwango vya usanifu wa mji rafiki kwa ndege vilianzishwa. Kanuni mpya za “kuzima taa kwa ajili ya ndege” zitaanza kutumika mapema Novemba mwaka huu. Hizi ni ishara za kwamba mji unajali kweli.
Kazi za urejeshaji mazingira ya asili zimekuwa kubwa. Zimeongeza zaidi ya hekta 30 za upandaji wa mikoko katika eneo pana la Ghuba ya Shenzhen, zimeboresha mabwawa ya samaki kuwa makazi mbalimbali ya kina kifupi na kirefu, zimeondoa spishi vamizi kama Sonneratia apetala ambazo zilikuwa zikikua haraka na kuchukua nafasi ya mimea ya asili, na zimeongeza uanuai wa viumbe vya chini ya maji kwa karibu asilimia 50.

Waandishi wa habari wakitazama viumbe wanaopatikana kwenye Hifadhi ya Kitaifa ya Mazingira ya Asili ya Guangdong Neilingding Futian mjini Shenzhen, mkoani Guangdong, China (People’s Daily Online)
Matokeo chanya ya kulinda ikolojia na ardhi oevu yanaonekana dhahiri. Nilikaa kwa muda fulani kwenye vituo na mnara wa kutazamia ndege, nikitazama kwa darubini. Wakati mwingine niliona ndege akitembea karibu sana, wakati mwingine kundi kubwa likiruka pamoja kama wingu. Nilihisi amani isiyo ya kawaida.
Katika mji kama Shenzhen, ambapo kila kitu kinaonekana kuwa cha maendeleo ya kasi na cha kisasa, mahali hapa kunakukumbusha kwamba mazingira ya asili yana midundo yake yenyewe. Niliwaza kuhusu watoto watakaokuja hapa baadaye, wakiwaona ndege hawa na kujifunza umuhimu wa kulinda mazingira. Pia niliwaza kuhusu changamoto zinazoendelea kuwepo—uchafuzi kutokana kwenye mji, mabadiliko ya tabianchi, na shinikizo la maendeleo—lakini nimehisi matumaini kwa sababu ya juhudi zinazoendelea.
Nmeondoka nikiwa kimya zaidi kuliko nilivyofika. Jua lilikuwa limeshuka kidogo, na rangi ya machweo ilianza kuonekana juu ya maji. Tofauti kati ya majumba ya glasi yaliyoangaza nyuma yangu na kazi ya uhimilivu wa mizizi, mawimbi, na mabawa inabaki nami. Ardhi oevu hii ndogo ya mjini si mabaki ya asili yaliyoachwa; ni udhihirisho wa makusudi na wenye nguvu hai kwamba mji wa kisasa bado unaweza kutoa nafasi kwa midundo ya mazingira ya asili ya dunia.

Meli hospitali ya jeshi la majini la China yawasili Cote d'Ivoire kutekeleza jukumu la matibabu

Tamasha la 19 la Utamaduni na Utalii la A-Ma lafunguliwa Macao, China

Utandazaji wa reli waanza kwenye reli ya mwendo-kasi ya Nantong-Ningbo mkoani Jiangsu, China

Mabaki ya vivutio vya kihistoria vya Safari Ndefu mkoani Sichuan, China
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma