Lugha Nyingine
Juu ya vilele vyenye theluji vya Golog: Mahali ambapo vitabu hufungua njia
Eneo Linalojiendesha la Watibeti la Golog katika Mkoa wa Qinghai kaskazini-magharibi mwa China, lipo kwenye mwinuko wa wastani wa mita zaidi ya 4,200 kutoka usawa wa bahari, jambo linalolifanya kuwa eneo linalojiendesha la kabila lililo kwenye mwinuko wa wastani wa juu zaidi nchini China.
Mazingira yake hayo ya mwinuko wa juu na baridi kali yameleta mandhari ya kuvutia ya Milima ya Amne Machin iliyofunikwa na theluji, lakini mazingira hayohayo pia yameleta changamoto za kipekee kwa maendeleo ya elimu katika eneo hilo la Golog.
"Golog ni moja ya maeneo yenye changamoto kubwa zaidi miongoni mwa maeneo 30 nchini China yanayojiendesha yenyewe na makabila madogo madogo, kwa vigezo vya mazingira yake ya asili," amesema Lu Ning, naibu mkurugenzi wa ofisi ya elimu ya eneo hilo.
Mwinuko huo wa juu, upungufu wa oksijeni, na watu wanaoishi kwa kutawanyika sana kwa muda mrefu vimekuwa vikikwamisha maendeleo ya elimu ya msingi katika eneo hilo. Matokeo yake ni kuwa kiwango cha elimu katika eneo hilo la Golog kiliwahi kuwa miongoni mwa viwango vya chini kabisa katika Mkoa wa Qinghai na nchini China kwa ujumla. Kwa wenyeji, elimu imekuwa moja ya masuala ya kimaisha yenye shinikizo zaidi.
Mwaka 2010, Mkutano wa Tano wa Kamati Kuu kuhusu Kazi zinazohusiana na Xizang uliiteua Shanghai kutoa usaidizi kwa Eneo hilo la Golog mkoani Qinghai. Ili kuvishinda vizuizi vya kijiografia katika elimu kwenye uwanda huo wa juu, Golog ilitumia mbinu bunifu ya kuendesha shule nje ya eneo hilo, na kuanzisha shule ya sekondari ya juu kwa ajili ya wanafunzi wa Golog katika mji wa Xining, mji mkuu wa mkoa wa Qinghai, ambako mwinuko ni wa chini zaidi. Mwaka 2019, Shule ya Sekondari ya Kabila ya Golog katika mji huo wa Xining ilikamilika na kuanza kudahili wanafunzi.
"Tunatumai kufungua kikamilifu uwezo wa kila mtoto kupitia elimu, ili kuwe na mwanga machoni mwao na ndoto mioyoni mwao," amesema Tian Zhe, mkurugenzi wa Ofisi ya Xining ya Serikali ya Mji wa Shanghai, ambaye pia ni mkuu wa kikundi cha uratibu kwa kundi la sita la maafisa waliotumwa kuiunga mkono Qinghai.
"Ili kufanikisha hili, tumeanzisha na kuleta kwa juhudi zote falsafa za hali ya juu za kielimu, rasilimali, na programu kutoka Shanghai na maeneo mengine ya China." Amesema Tian, ambaye pia ni naibu katibu wa Kamati ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ya Eneo hilo la Golog na naibu mkuu wa Eneo la Golog.
Kwa kuongozwa na mbinu hii, shule hiyo ilishirikiana na wahadhiri kutoka Chuo cha Muziki cha Shanghai kuanzisha bendi ya kwanza ya vijana wa kabila la Watibet ya China inayotumia ala za kupulizwa kwa mdomo; ambayo tangu kipindi hicho imeshatumbuiza katika Kituo cha Kitaifa cha Sanaa za Maonyesho mjini Beijing.
Shule hiyo pia imeanzisha kozi mpya za kisasa katika nyanja za AI, uvumbuzi wa kisayansi na kiteknolojia, pamoja na sayansi za majaribio halisia, na kutumia elimu ya sayansi na teknolojia ya hali ya juu kusaidia kupunguza pengo la kielimu kati ya maeneo ya mashariki mwa China na maeneo ya makabila madogo yaliyo magharibi mwa nchi hiyo.
Mwezi Juni 2024, wakati wa ziara ya ukaguzi katika Mkoa wa Qinghai, Rais wa China Xi Jinping—ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya CPC na Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Kijeshi ya China (CMC) —alitembelea Shule hiyo ya Sekondari ya Kabila ya Golog Xining. Alielezea matumaini yake kuwa wanafunzi watathamini mazingira mazuri ya shule hiyo. Alisisitiza kuwa wanapaswa kuwa na azma ya kuwa warithi na wajenzi wa mambo ya ujamaa wenye umaalum wa China, huku wakijitahidi kutengeneza fursa kwa ajili ya kujenga maendeleo bora na ya kipekee ya kitaaluma.
Zeng Qiang, mkuu wa Shule hiyo ya Sekondari ya Kabila ya Golog Xining, amesema kuwa kundi la kwanza la wanafunzi wa shule hiyo lilipofanya mtihani wa taifa wa kujiunga na vyuo, au gaokao mwaka 2022, asilimia zaidi ya 60 walifuzu kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza chuoni.
Katika mtihani wa gaokao uliomalizika hivi karibuni, idadi hiyo ilipanda hadi asilimia 84.17. Wanafunzi saba walifanikiwa kujiunga na vyuo vikuu vilivyo chini ya "Mradi 985," wanafunzi 38 walijiunga na vyuo vikuu vilivyo chini ya "Mradi 211," ambavyo vyote ni vyuo vikuu bora nchini China, na mmoja alijiunga na chuo cha kijeshi. Miaka ya juhudi imeleta maendeleo ya kihistoria ya kupiga hatua kubwa kwenye sekta ya elimu katika eneo hilo la Golog.
Xi amekuwa akisisitiza kuwa kuhakikisha watoto katika maeneo maskini wanapata elimu bora ni jukumu muhimu katika juhudi za kupunguza umaskini na kuleta maendeleo, vilevile ni njia muhimu ya kukata mnyororo wa kurithisha umaskini kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Zeng amesema kuwa uzoefu wake tangu alipofika Qinghai kupitia mpango huo wa usaidizi-sambamba, umempa uelewa wa kina zaidi wa umuhimu wa kufikia rasilimali bora za kielimu pamoja na mazingira mazuri ya kujifunzia.
"Wazazi wengi hawajawahi kamwe kutoka katika maeneo ya mbugani na milimani, isipokuwa tu pale wanapowaleta watoto wao Xining kwa ajili ya masomo. Mtoto anapoweza kutoka nje zaidi ya milima hiyo, pia inamaanisha familia nzima imepata fursa ya kuona dunia pana zaidi," amesema.
Ameongeza kuwa, katika kuendesha shule hiyo, msisitizo unawekwa kwenye kukuza maendeleo ya jumla ya wanafunzi—katika nyanja za maadili, akili, mwili, uerevu wa mambo, pamoja na elimu ya kazi.
"Tunaandaa ziara za kwenda ‘Mji wa Atomiki’ wa Qinghai ili wanafunzi wapate uzoefu wa moja kwa moja wa moyo wa mpango wa 'Mabomu Mawili, Satalaiti Moja'. Kwa uungaji mkono wa mpango wa usaidizi-sambamba wa Shanghai, tunawapeleka pia wanafunzi kwenye Mnara wa Oriental Pearl ili waone mandhari ya jiji kubwa la kisasa kutokea juu, na pia kwenye eneo ulikofanyika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa CPC, ili kujifunza kuhusu historia ya mapinduzi ya nchi hiyo mjini Shanghai," amesema.
"Tunatumai watoto hawa watakuwa na fursa za kutoka nje ya milima na kuona dunia pana zaidi, ili waweze kupata uelewa ulio wazi na kamili zaidi wa maendeleo ya mambo ya kisasa ya China. Kupitia kwao, tunatumai kufikia na kuleta athari chanya kwa watu wengine wengi zaidi," amesema Zou Hong'en, katibu mkuu wa kundi la uratibu kwa ajili ya kundi la sita la maafisa waliotumwa kuuunga mkono mkoa wa Qinghai.
Eneo la Sanjiangyuan mkoani Qinghai, linalojulikana kwa jina la "Mnara wa Maji wa China," ni eneo chimbuko la mito Yangtze, Manjano na Lancang. "Natumai watoto hawa watakuwa kama maji yanayotiririka kutoka Sanjiangyuan—wakisonga mbele kwa uhuru, huku wakirejesha manufaa kwa nchi yao," amesema Yang Wenbo, makamu mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kabila ya Golog Xining, akiongeza kuwa: "Kama tu Rais Xi alivyowahimiza, natumai watajitahidi kutengeneza fursa kwa ajili ya kujenga maendeleo bora na ya kipekee ya kitaaluma”.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



