Lugha Nyingine
Viongozi wa Ulaya wahoji mpango wa Trump wa kusimamisha mashambulizi ya nishati kati ya Russia na Ukraine

Picha hii iliyopigwa Septemba 17, 2026 ikionesha moshi ukifuka baada ya shambulizi la droni na kombora mjini Kiev, Ukraine. (Xinhua/Li Dongxu)
BRUSSELS – Viongozi wa Ulaya wamehoji kama Russia itaheshimu "makubaliano ya kusimamisha mashambulizi ya nishati" yaliyotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump, huku wakisema kuwa usitishaji halisi wa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati unaweza kuleta nafuu kama utatekelezwa.
Tangazo hilo, ambalo Moscow bado haijalithibitisha, limekuja wakati kukiwa na wasiwasi unaoongezeka barani Ulaya juu ya makubaliano hayo ya hivi karibuni ya Marekani na Russia ya kusambaza dizeli, pamoja na athari zake kwa vikwazo vya nchi za Magharibi na uhusiano wa pande za Bahari ya Atlantiki.

Picha hii iliyopigwa Machi 29, 2023 ikionyesha kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia kusini mwa Ukraine. (Picha na Victor/Xinhua)
Akizungumza jana Jumatatu mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, amesema kuwa umoja huo ungekaribisha hatua hiyo ya kusimamisha mashambulizi ya nishati kama ingetekelezwa, lakini amehoji kama Russia ingekubali kufanya hivyo.
"Tunakaribisha usimamishaji mashambulizi kwenye nishati utakapotekelezwa. Bado hatujaona kama Russia nayo itatilia maanani hilo," Kallas amewaambia waandishi wa habari kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya huko Luxembourg.
Amesema kuwa kusimamisha mashambulizi kwa kuzingatia tu viwanda vya kusafisha mafuta kungeinufaisha zaidi Russia, ambayo ina vituo vingi zaidi vya kusafisha mafuta kuliko Ukraine.
"Kama tunataka kumaliza vita hivi, njia pekee ya kufanya hivyo ni kuongeza shinikizo dhidi ya Russia," amesema Kallas, huku akitoa wito kwa Marekani kuiwekea vikwazo Moscow.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema Jumatatu kuwa hajaona dalili yoyote ya kusimamishwa kwa mashambulizi ya nishati kwa upande wa Russia, akitolea mfano wa kuendelea kwa mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine.
Waziri Mkuu wa Poland, Donald Tusk, pia ameeleza hali ya mashaka kuhusu uwezekano wa kusimamishwa kwa mashambulizi. Kwenye Jukwaa la Usalama la Warsaw, amesema Russia imekuwa ikikataa mara kwa mara mapendekezo ya kupunguza kupamba moto kwa vita.
Tusk pia ametoa wito wa kuimarishwa zaidi kwa vikwazo dhidi ya Russia.
Ukosoaji wa Ulaya pia umejikita katika makubaliano ya Washington na Moscow kuhusu usambazaji wa dizeli.
Chansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema kwamba makubaliano ya dizeli kati ya Marekani na Russia "hayakuwa sehemu ya mjadala" kwa Ujerumani na Ulaya.
“Russia inaweza tu kujadiliana kwa uzito chini ya shinikizo,” amesema. Ameeleza kuwa Ujerumani itadumisha vikwazo vyake dhidi ya Moscow, na ametoa wito wa kuchukua hatua kali zaidi kufuatia kuendelea kwa mashambulizi ya Russia kwenye miundombinu ya nishati ya Ukraine.

Rais wa Marekani Donald Trump (kulia) akihutubia mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Rais wa Russia Vladimir Putin baada ya kumaliza mazungumzo yao huko Anchorage, Alaska, Marekani, Agosti 15, 2025. (Xinhua/Wu Xiaoling)

Picha hii iliyopigwa Machi 18, 2025 ikionesha mandhari ya Kremlin mjini Moscow, mji mkuu wa Russia. (Xinhua/Bai Xueqi)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



