Lugha Nyingine
Wahouthi na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen washambuliana upya huku wasiwasi ukiongezeka kimataifa
Wafuasi wa Wahouthi wakishiriki kwenye mkutano wa hadhara wa kijeshi ulioandaliwa kupinga ushiriki wa Uturuki, Pakistan na Saudi Arabia kwenye mgogoro wa Yemen, mjini Sanaa, Yemen, Oktoba 7, 2026. (Picha na Mohammed Mohammed/Xinhua)
RIYADH/SANAA - Mapigano kati ya Wahouthi wa Yemen na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia yameonesha dalili za kutopungua jana Jumapili kutokana na mashambulizi mapya kupiga viwanja vikubwa vya ndege nchini Saudi Arabia, huku kundi hilo la Wahouthi likidai kufanya operesheni mpya za makombora na droni dhidi ya viwanja vya ndege na vituo vya nishati vya Saudi Arabia na muungano huo ukiapa kuchukua hatua kali za kulipiza.
Mamlaka Kuu ya Usafiri wa Anga ya Saudi Arabia (GACA) imesema jana Jumapili kwamba shambulizi jipya kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Khalid katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, limesababisha majeruhi. Mapema siku hiyo, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulisema kombora lisilojulikana lilipiga kituo cha abiria kwenye uwanja huo wa ndege, na moto uliotokana na shambulizi hilo ulikuwa ukidhibitiwa katika eneo hilo.
Katika taarifa ya baadaye, GACA imesema Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Fahd karibu na Dammam katika Jimbo la Mashariki ulishambuliwa Jumapili jioni, huku tathmini za uharibifu na ukaguzi wa usalama wa miundombinu ya uwanja wa ndege ukiendelea.
Kundi hilo la Wahouthi limedai kuwa limefanya operesheni nne za makombora na droni dhidi ya viwanja vya ndege na miundombinu ya nishati katika sehemu mbalimbali za Saudi Arabia katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Wakati huo huo, mashambulizi ya anga ya Saudi Arabia yaliendelea katika maeneo mbalimbali yanayoshikiliwa na Wahouthi nchini Yemen, huku muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ukiapa kujibu vikali mashambulizi hayo ya Wahouthi.
Msemaji wa jeshi la Wahouthi Yahya Sarea amedai kuwa ndege za kivita za Saudi Arabia zilifanya mashambulizi ya anga 124 katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Mgogoro huo unaozidi kupamba moto umeibua wasiwasi mkubwa kimataifa, hasa baada ya shambulizi hilo la Wahouthi dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Khalid mjini Riyadh siku ya Jumamosi kusababisha vifo vya watu 12 na kujeruhi wengine 309.
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sudan, Misri, Uturuki, Israel, Iraq, Syria, Palestina, Bahrain na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pia zimelaani shambulizi hilo la Jumamosi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



