Lugha Nyingine
Tetemeko kubwa la ardhi na mitetemo ya baada yake vyatikisa Panama huku mamlaka zikichukua hatua za dharura

Picha ikionesha jengo lililobomoka kufuatia tetemeko la ardhi, Sona, Jimbo la Veraguas, Panama, tarehe 9 Oktoba 2026. (Xinhua)
PANAMA CITY - Tetemeko kubwa la ardhi na mfululizo wa mitetemo mikali iliyofuata vimeitikisa Panama jana Ijumaa, na kusababisha wakazi kukimbilia mitaani, huduma ya maji kutatizika na safari za ndege kusimamishwa kwa muda mfupi huku serikali ikikusanya wafanyakazi wa dharura na rasilimali kwa kukabiliana na hali hiyo.
Taasisi ya Sayansi ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Panama imepima ukubwa wa tetemeko la awali kuwa 7.2. Lilitokea saa 6:56 mchana kwa saa za huko (1756 GMT), likiwa na kina cha kilomita 4. Hadi kufikia saa 11:30 jioni kwa saa za huko, matetemeko zaidi ya 40 yalikuwa yamerekodiwa, yakiwemo matetemeko zaidi ya 12 yenye ukubwa wa zaidi ya 5.0. Tetemeko moja lilitokea saa 9:25 jioni likiwa na ukubwa wa 6.9.
Shirika la Utafiti wa Kijiolojia la Marekani (USGS) mwanzoni liliripoti kuwa tetemeko la kwanza lilikuwa na ukubwa wa 8, kisha likarekebisha kipimo hicho hadi 7.6 na baadaye hadi 7.7.
Katika Panama City, umati wa watu ulitoka kwenye majengo na kukusanyika kando ya barabara na katika maeneo ya wazi. Baadhi ya watu walishindwa kuzuia hisia zao wakati wakieleza jinsi ardhi ilivyotikisika, huku wengine wakitokwa machozi.
"Lilikuwa na nguvu sana. Hata jengo lilikuwa likiyumba," amesema Tina Smith, ambaye alikuwa nje pamoja na wafanyakazi wenzake. Amesema kuwa wote walikuwa salama.
Hali hiyo ya awali ya taharuki ilipungua taratibu, lakini mitetemo ya mara kwa mara ya baada yake iliwafanya watu wengi kubaki nje. Baadhi ya maeneo ya umma yalifungwa, msongamano wa magari ulitokea katika barabara kadhaa, na wakazi wa majengo marefu walisema waliogopa kurejea nyumbani.
Rais wa Panama, Jose Raul Mulino, amesema ameziagiza taasisi husika kuripoti haraka athari za tetemeko hilo na kupeleka wafanyakazi, rasilimali, na misaada kwa jamii zilizoathirika. Amesema serikali nzima imekusanya nguvu zake na kwamba yeye binafsi atashiriki katika juhudi za kukabiliana na athari zake na kuratibu shughuli hizo katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Jengo lililoharibika likionekana baada ya tetemeko la ardhi, Sona, Jimbo la Veraguas, Panama, Oktoba 9, 2026. (Xinhua)

Jengo liliharibika likionekana baada ya tetemeko la ardhi, Sona, Jimbo la Veraguas, Panama, Oktoba 9, 2026. (Xinhua)

Watu wakiwa wamekusanyika nje baada ya tetemeko la ardhi, Panama City, Panama, Oktoba 9, 2026. (Xinhua/Li Jiaxu)

Magari yakiendeshwa barabarani baada ya tetemeko la ardhi, Panama City, Panama, Oktoba 9, 2026. (Xinhua/Li Jiaxu)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



