Lugha Nyingine
Putin na Trump wafanya mazungumzo kwa simu juu ya mgogoro wa Ukraine na usambazaji nishati
MOSCOW/WASHINGTON - Rais wa Russia Vladimir Putin amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Ijumaa, ambapo katika mazungumzo hayo kwa sehemu kubwa walijikita kwenye uwezekano wa kutatua mgogoro wa Ukraine, Kremlin imesema katika taarifa yake.
Kwa mujibu wa Kremlin, juu ya suala la mwenendo wa nishati duniani, Russia imesisitiza tena utayari wake wa kusambaza mafuta ghafi na bidhaa za petroli katika masoko ya Marekani na dunia nzima.
"Nina imani kuwa hili litakuwa na matokeo chanya kwa uchumi mzima wa dunia," Putin amesema.
Habari zimesema mazungumzo hayo pia yaligusia hali kuhusu Iran na mambo mbalimbali ya uhusiano wa pande mbili ambapo pande hizo mbili zimesisitiza dhamira zao katika kudumisha mawasiliano ya kibinafsi kati ya marais hao na kuendeleza ushirikiano kati ya serikali zao, mashirika ya ujasusi na mashirika mengine.
Trump pia amethibitisha kufanyika kwa mazungumzo hayo kwa njia ya simu kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social.
"Nimemaliza punde mazungumzo yenye mafanikio makubwa na Rais Vladimir Putin wa Russia, ambapo imekubaliwa kuwa Russia itasambaza mara moja tani zaidi ya 300,000 za mafuta ya dizeli kwenye soko la Marekani na dunia, tani nyingine 500,000 katika mwezi wa Novemba, na tani 1,000,000 mara tu baada ya hapo," Trump ameandika.
"Aidha, kulingana na hali ya viwanda vyao vya kusafisha dizeli, Russia itawasilisha, ndani ya kipindi kifupi cha muda, tani 3,000,000 za mafuta ya dizeli," ameongeza.
Trump ameeleza imani yake kuwa usambazaji huo utasaidia kushusha bei ya dizeli duniani kwa haraka.
Kufuatia mazungumzo hayo, Naibu Waziri Mkuu wa Russia Alexander Novak amesema kuwa Russia itaanza kuondoa vizuizi vya usafirishaji wa dizeli nje ya nchi kabla ya muda uliopangwa.
Siku hiyo hiyo, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitoa kibali cha muda cha jumla kinachoruhusu uuzaji, uwasilishaji, upakuaji na uingizaji wa dizeli inayotoka Russia kwenye soko la dunia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



