Lugha Nyingine
Watu 44 wauawa katika mapigano kati ya jeshi la serikali ya Yemen na kundi la Wahouthi
Watu wasiopungua 44 kutoka jeshi la serikali ya Yemen na wapiganaji wa kundi la Wahouthi wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mapigano makali yaliyotokea mapema Jumatatu katika Jimbo la kusini la Lahj karibu na Mlango Bahari wa kimkakati wa Bab al-Mandab, kwa mujibu wa vyanzo viwili vya pande hizo mbili zinazopigana.
Kwa mujibu wa ofisa wa jeshi la Yemen ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mapigano hayo yalitokea baada ya wapiganaji wa kundi la Wahouthi kuanzisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya milimani yanayodhibitiwa na serikali katika wilaya ya Al-Madaribah wa Ras Al-Arah, eneo la miamba lenye miinuko linalotazama njia zinazoelekea Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab.
Pia siku hiyo ya Jumatatu, chanzo cha kijeshi ndani ya kundi la Wahouthi, kikizungumza na Xinhua kwa sharti la kutotajwa jina, kilisema wapiganaji wa Wahouthi wamewaua wanajeshi 16 wa serikali na kujeruhi wengine kadhaa katika mapigano hayo huko Lahj.
Mapigano yamekuwa yakipamba moto katika maeneo ya kusini-magharibi mwa Yemen hivi karibuni baada ya kundi hilo kuteka mji muhimu wa bandari wa Mocha na Kisiwa cha Mayyun kwenye Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab mapema mwezi huu.
Mgogoro wa Yemen ulianza mwishoni mwa mwaka 2014 wakati Wahouthi walipoteka mji mkuu wa Sanaa na sehemu kubwa ya kaskazini mwa Yemen, hatua iliyosababisha muungano unaoongozwa na Saudi Arabia kuingilia kati mwezi Machi 2015 ili kuiunga mkono serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



