Lugha Nyingine
Mjadala wa FAO na China kuhusu mifumo ya mali za urithi wa kilimo yafunguliwa nchini Afrika Kusini

Jeremie Mbairamadji, mratibu mwandamizi wa Sekretarieti ya Mifumo Muhimu ya Mali za Urithi wa Kilimo Duniani (GIAHS) ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), akizungumza kwenye mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua, Johannesburg, Afrika Kusini, tarehe 28 Septemba 2026. (Xinhua/Chen Wei)
JOHANNESBURG - Mjadala wa siku tatu kuhusu kujenga uwezo wa Mifumo Muhimu ya Mali za Urithi wa Kilimo Duniani (GIAHS) barani Afrika umefunguliwa jijini Johannesburg, Afrika Kusini jana Jumatatu, mjadala huo unalenga kuongeza uelewa na kuimarisha usimamizi wa mali za urithi wa kilimo barani Afrika.
Maofisa wa serikali, wajumbe wa vituo vya mawasiliano vya nchi mbalimbali, wataalamu kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), taasisi za utafiti, na mashirika ya kiraia kutoka nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya Kiingereza wamekusanyika pamoja kwenye mjadala huo.
Mjadala huo umepata ufadhili wa mradi wa Ushirikiano wa Kusini-Kusini kati ya FAO na China, unawapa washiriki ujuzi na ufundi wa kazi na vyombo vya matumizi halisi vinavyowasaidia kuandaa miswada ya miradi ya GIAHS na kupata fursa za ufadhili. Mjadala kama huo pia utafanyika katika nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya Kifaransa.
Jeremie Mbairamadji, mratibu mwandamizi wa Sekretarieti ya GIAHS ya FAO, amesisitiza umuhimu wa kuongeza maeneo ya mifumo muhimu ya mali za urithi wa kilimo yaliyobainishwa barani Afrika, akieleza kuwa kati ya maeneo zaidi ya 140 yanayotambuliwa duniani, Afrika ina maeneo 4 tu kwa sasa. Asia inaongoza duniani kwa kuwa na maeneo 65, ambayo mengi kati yake yako nchini China.
Mbairamadji amepongeza uungaji mkono wa siku zote wa China kwa ujengaji uwezo na uhamishaji wa ujuzi na ufundi wa kazi, na amesema kuwa kila mwaka China inaandaa miradi ya utoaji mafunzo ya kiwango cha juu kualika washiriki wa kimataifa kufanya ziara za kubadilishana uzoefu, na kuunga mkono Sekretarieti ya GIAHS katika kueneza uzoefu bora zaidi.
Du Lei, konsuli katika Ubalozi wa China nchini Afrika Kusini, amesisitiza ahadi ya China ya kushirikiana na FAO kusaidia nchi za Afrika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Du Lei, Konsuli katika Ubalozi wa China nchini Afrika Kusini, akizungumza kwenye mahojiano na shirika la habari la China, Xinhua, Johannesburg, Afrika Kusini, tarehe 28 Septemba 2026. (Xinhua/Chen Wei)
Morongoa Leseke, mkurugenzi mkuu katika Idara ya Misitu, Uvuvi na Mazingira ya Afrika Kusini, amekaribisha mpango huo wakati huu ambapo Afrika Kusini inasukuma mbele mpango wake wa kitaifa wa upandaji miti. Amesisitiza umuhimu wa kujifunza kutoka kwa China kuhusu teknolojia ya hali ya juu ya kilimo na ameeleza matumaini ya kushirikiana na FAO katika kutoa mafunzo kuhusu ujuzi na ufundi wa kilimo na misitu.

Morongoa Leseke, mkurugenzi mkuu katika Idara ya Misitu, Uvuvi na Mazingira ya Afrika Kusini, akizungumza kwenye mahojiano na shirika la habari la China, Xinhua, Johannesburg, Afrika Kusini, tarehe 28 Septemba 2026. (Xinhua/Chen Wei)

Picha hii iliyopigwa tarehe 28 Septemba 2026 ikionyesha mandhari kwenye mjadala wa kikanda wa kujenga uwezo wa Mifumo Muhimu ya Mali za Urithi wa Kilimo Duniani (GIAHS) barani Afrika, jijini Johannesburg, Afrika Kusini. (Xinhua/Chen Wei)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



