Lugha Nyingine
Michezo ya Asia | China yanyakua medali tatu za dhahabu huku Boonson akipata rekodi sawa na ile ya Asia ya mbio za mita 200

Puripol Boonson wa Thailand akishangilia baada ya fainali ya mbio za mita 200 kwa wanaume kwenye Michezo ya Asia 2026 jijini Nagoya, Japan, Septemba 27, 2026. (Xinhua/Jia Yuchen)
NAGOYA, Japan - Puripol Boonson wa Thailand amepata rekodi sawa na ile ya Asia ya sekunde 19.88 katika mbio za mita 200 kwa wanaume, na timu ya China imenyakua medali tatu za dhahabu katika mashindano ya mbio za mita 110 za kuruka viunzi kwa wanaume, kuruka mbali kwa wanawake na kurusha mkuki kwa wanawake kwenye Michezo ya Asia 2026 jijini Nagoya, Japan jana Jumapili.
Chen Yuanjiang alishinda mbio za mita 110 kuruka viunzi kwa wanaume baada ya kutumia muda wa sekunde 13.15, huu ni ushindi wa mara nyingine tena kwa timu ya China katika mchezo huo baada ya miaka minane iliyopita. Rachid Muratake wa Japan alishinda medali ya fedha, na John Tolentino wa Ufilipino ameshinda medali ya shaba.
Katika mashindano ya kurusha mkuki kwa wanawake, mshikiliaji rekodi ya Asia, Yan Ziyi, alirusha mkuki kwa umbali wa mita 70.46 katika jaribio lake la kwanza tu akinyakua medali ya dhahabu. Bingwa wa Olimpiki Haruka Kitaguchi wa Japan ameshinda medali ya fedha kwa kurusha umbali wa mita 62.70.

Yan Ziyi wa China akishiriki kwenye fainali ya kurusha mkuki kwa wanawake. (Xinhua/Luo Yuan)
Matokeo hayo ya Yan pia yamevunja rekodi ya Michezo ya Asia ya mita 66.09 iliyowekwa na mwanamichezo mwenzake Liu Shiying ambaye alikuwa mshindi wa China wa medali ya Michezo ya Olimpiki.
"Nimefurahi sana, na siwezi kusubiri kusikia muziki wa wimbo wa taifa ukipigwa," alisema.

Mshindi wa medali ya dhahabu Yan Ziyi (kushoto) wa timu ya China akiwa na kocha wake baada ya mashindano ya kurusha mkuki kwa wanawake. (Xinhua/Jia Yuchen)
Katika mbio za mita 200 kwa wanawake, Shanti Pereira wa Singapore alikimbia kwa muda wa sekunde 22.78—muda wake bora zaidi msimu huu—na kutetea taji lake la Michezo ya Asia, wakati Chen Yujie wa China, mwenye umri wa miaka 17 aliyeshinda mbio za mita 100 kwa rekodi ya michezo hiyo ameshinda medali ya fedha kwa kukimbia kwa muda wa sekunde 22.93.

Chen Yujie wa China akishangilia baada ya fainali ya mbio za mita 200 kwa wanawake. (Xinhua/Jia Yuchen)
Boonson amepata rekodi sawa na ile ya Asia iliyowekwa na Xie Zhenye wa China mwaka 2019 kwa kukimbia kwa sekunde 19.88 katika fainali ya mbio za mita 200 kwa wanaume. Huang Youwen wa China, mwenye umri wa miaka 21, alishinda medali ya fedha kwa kutumia muda wa sekunde 20.45.
Katika mashindano ya kuruka mbali kwa wanawake, Huang Yingying wa China alikuja kutoka nyuma kwa kuruka mita 6.55 katika raundi ya sita ya mwisho, na kumshinda Ancy Sojan Edappilly wa India kwa tofauti ya sentimita mbili na kunyakua medali ya dhahabu. Mchina mwingine Tan Mengyi, ameshinda medali ya shaba kwa kuruka mita 6.46.

Huang Yingying wa China akishiriki kwenye fainali ya kuruka mbali kwa wanawake. (Xinhua/Luo Yuan)
Huang pia alishindana kwenye mashindano ya kuruka mara tatu (triple jump) siku ya Alhamisi na kushinda medali ya fedha.
Katika mashindano ya kuruka juu kwa wanaume, Fu Chao-hsuan wa Taipei ya China amepata medali ya dhahabu kwa kuruka urefu wa mita 2.25 na kumshinda Sarvesh Kushare wa India . Mutaz Barshim wa Qatar, mshindi wa medali ya Olimpiki mwenye umri wa miaka 35, alijitoa kwenye fainali hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



