Lugha Nyingine
Vucic ajiuzulu wadhifa wa Rais wa Serbia

Rais wa Serbia Aleksandar Vucic akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Belgrade, Serbia, tarehe 27 Septemba 2026. (Picha na Predrag Milosavljevic/Xinhua)
BELGRADE - Rais wa Serbia Aleksandar Vucic ametia saini na kuwasilisha barua ya ombi lake la kujiuzulu na kuachia wadhifa wa urais jana Jumapili. "Sasa ninatia saini waraka huu kama ufuatao: 'Kwa mujibu wa kifungu cha 116, ibara ya 5 ya Katiba ya Nchi ya Jamhuri ya Serbia, nimewasilisha ombi langu la kujiuzulu wadhifa wa Rais wa Jamhuri.'...Ana, waraka huu ungewasilishwa Bungeni, na kesho unaenda kwenye makabidhiano ya madaraka," amesema Vucic wakati huohuo akimtaja Ana ambaye ni Spika wa Bunge la Serbia.
Kwa mujibu wa Katiba ya Nchi ya Serbia na Sheria ya Urais, kipindi cha rais madarakani hukamilika barua ya ombi la kujiuzulu inapopokelewa rasmi na Bunge la Taifa, bila kuhitaji kuidhinishwa na Bunge. Spika wa Bunge la Taifa, Ana Brnabic, kisha atachukua wadhifa wa urais kwa muda wa hadi miezi mitatu, na katika wakati huu ambapo lazima aitishe uchaguzi wa rais ndani ya kipindi hicho.Vucic pia amesema atashiriki akiwa raia wa kawaida katika uchaguzi wa mapema wa bunge uliopangwa kufanyika tarehe 25 Oktoba.
Bunge la Serbia lilivunjwa Septemba 9. Kwa mujibu Katiba ya Nchi, bunge lililovunjwa huwa na mamlaka yaliyopunguzwa, wakati huohuo serikali inaendelea na wajibu wake wa kutekeleza majukumu hadi serikali mpya itakapoundwa.
Septemba 5, Chama cha Maendeleo cha Serbia (SNS) kilimteua Vucic kuwa wa kwanza kwenye orodha ya wagombea wake wa nafasi ya Waziri Mkuu katika uchaguzi huo wa mapema wa bunge.
Baada ya uchaguzi wa Oktoba 25, utaratibu wa kuunda serikali mpya utaanza kutekelezwa. Kaimu rais, baada ya kushauriana na wajumbe wa orodha za wagombea walioshinda, atapendekeza mgombea mteule wa Waziri Mkuu kwa Bunge la Taifa. Kisha mgombea mteule huyo anawasilisha mpango wa serikali na majina ya wajumbe wa baraza la mawaziri, na hayo yote lazima yaidhinishwe kwa wingi wa wabunge wote.
Vucic, aliyezaliwa Belgrade mwaka 1970, aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi, Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza, na Waziri Mkuu. Alichaguliwa kuwa rais mwaka 2017 na kuchaguliwa tena mwaka 2022.
Kwa mujibu wa Katiba ya Nchi ya Serbia, muda wa kushika madaraka ya urais ni miaka mitano, na kila rais anaruhusiwa kushika madaraka kwa awamu mbili tu.

Rais wa Serbia Aleksandar Vucic akihudhuria mkutano na waandishi wa habari mjini Belgrade, Serbia, tarehe 27 Septemba 2026. (Picha na Predrag Milosavljevic/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



