China na Marekani zafikia matokeo na maelewano manane katika ziara ya Rais Xi

(CRI Online) Septemba 28, 2026

Kuanzia tarehe 23 hadi 25 Septemba, Rais Xi Jinping wa China alifanya ziara ya kiserikali nchini Marekani. Kwenye ziara hiyo, marais wa nchi mbili hizo walibadilishana maoni kwa kina kuhusu uhusiano wa kiujenzi kati ya China na Marekani wenye utulivu wa kimkakati, na masuala makubwa ya kimataifa na kikanda, na kufikia matokeo na maelewano manane yafuatayo:

Kwanza; pande zote mbili zimekubaliana kujenga "uhusiano wa kiujenzi kati ya China na Marekani wenye utulivu wa kimkakati kwa msingi wa kuheshimiana, haki na usawa".

Pili; China na Marekani zimekubaliana kuungana mkono katika kuandaa kwa mafanikio Mkutano wa Viongozi wa Uchumi wa APEC na Mkutano wa Viongozi wa G20. Imekubaliwa kuwa, marais hao wawili wana nia ya kuhudhuria mikutano itakayoandaliwa na upande mwingine.

Tatu; marais wa nchi hizo mbili wamekubaliana kwamba Iran inapaswa kutimiza ahadi yake ya kutoendeleza silaha za nyuklia na kwamba hakuna nchi au taasisi inayopaswa kuweka tozo kwenye njia za maji za kimataifa.

Nne; marais hao wawili wamekumbusha kuwa China na Marekani zilikuwa washirika kwenye Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na zilipigana bega kwa bega ili kushinda vita hivyo.

Tano; marais hao wawili wametambua mchango chanya wa mfumo wa mashauriano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani na kuunga mkono matokeo ya mashauriano kati ya ujumbe wa kiuchumi na kibiashara wa nchi hizo mbili—ikiwemo kuanzisha na kusukuma mbele Bodi ya Biashara na mifumo mingine, na mpangilio kwa ajili ya kupunguziana ushuru wa bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 30, na kurefusha muda wa matokeo ya mazungumzo ya kiuchumi na kibiashara ya Kuala Lumpur—wakitoa maelekezo kwamba matokeo hayo yatekelezwe.

Sita; ushirikiano kati ya vyombo vya mapambano dhidi ya dawa za kulevya na vyombo ya kusimamia utekelezaji wa sheria vya China na Marekani umepata matokeo halisi. Hivi karibuni, pande hizo mbili zimeshirikiana kwa karibu kukabiliana na kesi kadhaa zinazohusisha aina mpya za dawa zinazoathiri mfumo wa fahamu (psychoactive substances) na kemikali zinazotumika kutengeneza dawa hizo, na kukamata washukiwa kadhaa wa uhalifu katika nchi zote mbili.

Saba; pande zote mbili zimekubaliana kuanzisha mazungumzo kati ya China na Marekani juu ya AI ili kubadilishana maoni kuhusu hatari na faida zinazohusiana na teknolojia hiyo. Mazungumzo yajayo yatafanyika mwezi Novemba mwaka huu. Pande zote mbili zimekubaliana kuanzisha njia ya mawasiliano kwa ajili ya matukio yanayohusiana na AI.

Nane; Marekani imekaribisha kuwasili kwa panda wawili waliokodishwa na China katika Bustani ya Wanyama ya Atlanta.

Aidha, majeshi ya China na Marekani yamekubaliana kukamilisha kumbukumbu ya maelewano kuhusu mawasiliano na kuzuia hatari za dharura mapema iwezekanavyo, na kuendeleza ushirikiano wao katika kutafuta miili ya wanajeshi wa Marekani ambayo haijulikani ilipo.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha