Lugha Nyingine
11 wameuawa, na wengine watatu wamejeruhiwa katika tukio la ufyatuaji risasi nchini Afrika Kusini

Picha hii iliyopigwa Septemba 23, 2026 inaonyesha eneo la tukio la ufyatuaji risasi huko KwaMakhutha katika Mkoa wa KwaZulu-Natal, Afrika Kusini. (Picha na Mbuthi Msweli/Xinhua)
Polisi wa Afrika Kusini wamesema watu 11 wameuawa na wengine watatu wamejeruhiwa kwenye tukio la ufyatuaji risasi lililotokea jumanne huko KwaMakhutha katika Mkoa wa KwaZulu-Natal kusini-mashariki mwa Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Polisi wa mkoa huo (SAPS), ufyatuaji risasi huo ulitokea Jumanne usiku katika eneo la Ziko. Wanaume watatu walifika na kuwafyatulia risasi wanaume 13 na mwanamke anayeaminika kuwa mjamzito walipokuwa wakiwa kwenye sherehe ndani ya nyumba. Polisi walisema watu 10, akiwemo mwanamke huyo, walifariki papo hapo kwa kupigwa risasi, na wengine wanne walipelekwa hospitali, mmoja wao alifariki baadaye kutokana na majeraha ya risasi, na kufanya idadi ya vifo kufikia 11.
Kaimu Kamishna wa polisi, Puleng Dimpane ameamuru kuanzishwa mara moja kwa operesheni ya kufuatilia ya saa 72 ili kuwakamata washukiwa. Amesema kwenye taarifa kuwa, "Polisi lazima wachukue hatua haraka, kuhamasisha rasilimali zote zinazopatikana na kuwafuatilia waliohusika hadi watakapofikishwa mahakamani."
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa baadhi ya wahanga walikuwa wakifuatiliwa na Idara ya Ujasusi ya Uhalifu ya SAPS kwa sababu ya kuhusika na shughuli zinazodaiwa kuwa haramu, polisi wamesema bila kutoa maelezo zaidi. Wamesema sababu ya ufyatuaji risasi bado haijathibitishwa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



