Marekani, Denmark na Greenland zasaini makubaliano ya kupanua uwepo wa kijeshi wa Marekani huko Greenland

(CRI Online) Septemba 23, 2026

Marekani, Denmark na eneo lake inalomiliki la Greenland wamesaini makubaliano mjini New York siku ya Jumanne ya kupanua uwepo wa kijeshi wa Marekani katika kisiwa hicho cha kimkakati cha eneo la Aktiki.

Katika hafla iliyofanyika kando ya Mjadala Mkuu wa Umoja wa Mataifa, makubaliano hayo yalisainiwa na Rais wa Marekani Donald Trump, Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen na Waziri Mkuu wa Greenland Jens-Frederik Nielsen.

Chini ya makubaliano hayo mapana, Marekani itaruhusiwa kuboresha na kupanua shughuli zake katika Kituo cha Anga cha Pituffik, ambacho tayari inakiendesha kaskazini-magharibi mwa Greenland, na kuanzisha eneo jingine la ulinzi huko Narsarsuaq na Mestersvig.

Makubaliano hayo pia yanaruhusu ndege za Marekani kuruka na kutua katika eneo lolote la Greenland, ikiwemo eneo lake la maji. Makubaliano hayo yanazuia mataifa yasiyo ya NATO kuanzisha vituo vya kijeshi vyenye wanajeshi au visivyo na wanajeshi huko Greenland. Pia yanazuia mataifa yasiyo ya NATO na yasiyo ya Umoja wa Ulaya kudhibiti sekta nyeti za eneo hilo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha