Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa laanza mjadala mkuu

(CRI Online) Septemba 23, 2026

Mjadala Mkuu wa kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ulifunguliwa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York siku ya Jumanne.

Rais wa kikao cha 81 cha Baraza Kuu, Khalilur Rahman, aliongoza ufunguzi wa mjadala huo, ambao ulikuwa chini ya mada "Kurejesha uaminifu, kusimamia mageuzi: Umoja wa Mataifa unaowahudumia wote". Katika hotuba yake ya ufunguzi, Rahman alisisitiza umuhimu wa kujenga upya uaminifu, akisema uaminifu hautolewi bali unapatikana. Amesisitiza kuwa uaminifu unapatikana kwa njia tatu: kwanza, kwa kukubali kwa dhati uhalisia kuhusu wapi tulipoachwa nyuma; pili, kwa kuangalia msingi wa mageuzi ya Umoja wa Mataifa ili kutoa matokeo bora; na tatu, kwa kufanya kazi iwe jumuishi zaidi na kuwashirikisha wadau wote husika, kutoka sehemu zote za jamii.

Katika ripoti yake ya "hali ya dunia" kabla ya ufunguzi wa Mjadala Mkuu wa mwaka huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kuwepo kwa dunia yenye ncha nyingi zilizounganishwa, badala ya kuwa na ile iliyogawanyika na inayofuata diplomasia ya mabadilishano ya maslahi (transactionalism).

Guterres alisema dunia yenye ncha nyingi zilizounganishwa inaweza kuweka mazingira ya kutatua matatizo ya kimataifa kwa njia ya uwiano na inayowakilisha wadau mbalimbali, lakini inahitaji mfumo wa ushirikiano wa pande nyingi ambao kiini chake ni Umoja wa Mataifa wenye uwiano na uwakilishi, yaani taasisi imara na madhubuti zinazoakisi uhalisia na mabadiliko ya taratibu ya uzito wa nchi na uchumi katika dunia ya sasa, na wala sio mifumo ya madaraka ya miaka 80 iliyopita.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha