Uganda yawataka wakulima wa kahawa kuwa imara licha ya changamoto za soko na hali ya hewa

(CRI Online) Septemba 22, 2026

Serikali ya Uganda imewataka wakulima wa kahawa wasitake tamaa kwa sababu ya kuyumba kwa soko la dunia na hali mbaya ya hewa inayoathiri uzalishaji.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Frank Tumwebaze, kwenye taarifa iliyotolewa Jumapili. Amebainisha kuwa soko la kimataifa la kahawa hivi karibuni limekabiliwa na shinikizo la kushuka kwa bei kutokana na ongezeko la usambazaji kutoka nchi kuu zinazozalisha kahawa, hasa Brazil na Vietnam. Aidha, alisema Uganda inakabiliwa na changamoto za usambazaji wa ndani kufuatia kipindi kirefu cha ukame na viwango vya juu vya joto visivyo vya kawaida katika maeneo kadhaa yanayolima kahawa.

Kwa mujibu wa waziri huyo, Uganda iliuza nje ya nchi magunia 846,376 ya kahawa (yenye uzito wa kilo 60 kila moja) mwezi Julai 2026, idadi ambayo ni pungufu ikilinganishwa na magunia 997,105 yaliyouzwa mwezi kama huo mwaka uliopita. Mapato yatokanayo na mauzo ya kahawa nje ya nchi pia yameshuka kutoka dola milioni 250.7 mwezi Julai 2025 hadi dola za Marekani milioni 204.1 mwezi Julai 2026.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha