Lugha Nyingine
Daktari wa China amsaidia mwanafunzi msichana wa Zanzibar kurejesha afya yake na kurudi tena shuleni

Picha hii inamwonesha Ashfaina Omari Ali (katikati, mbele) akiwa pamoja na Daktari Li Li (wa kwanza kulia, mbele) wa timu ya 35 ya madaktari wa China visiwani Zanzibar, wakati wa ziara ya ufuatiliaji kabla ya kurejea shuleni Zanzibar, Tarehe 7 Septemba 2026. (Timu ya 35 ya Madaktari wa China Zanzibar/Picha imetolewa na Xinhua)
Jumanne asubuhi, Ashfaina Omari Ali mwenye umri wa miaka tisa na nusu, aliingia tena Shule ya Msingi Sebleni kisiwani Unguja, Zanzibar, akiwa na hali mpya ya kujiamini. Kurejea shuleni kwa Bi. Ashfaina, kulikuwa ni ishara kwamba maisha yake yalikuwa yanarudi katika hali ya kawaida, baada ya ugonjwa wa sikio kutishia afya yake na kuathiri masomo yake.
Kupona kwa Ashfaina kulitokana na upasuaji wenye utatanishi uliofanywa katika Hospitali ya Lumumba, Zanzibar, na timu ya madaktari kutoka China ikiongozwa na daktari Li Li wa timu hiyo ya 35 ya madaktari wa China waliopo Zanzibar.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka tisa alikuwa anasumbuliwa na homa na kifafa vinavyojirudiarudia. Hapo awali, alipata matibabu ya kawaida ya kupunguza uvimbe katika kituo cha afya cha eneo hilo, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya.
Alipohamishiwa katika Hospitali ya Lumumba, Daktari Li na timu yake walifanya vipimo vya picha za ndani ya mwili na kugundua kuwa alikuwa na tatizo la kuzaliwa nalo la cholesteatoma ya sikio, hali mbaya inayohusisha ukuaji usio wa kawaida wa ngozi ndani ya sikio la kati.
Madaktari hao walitathmini kwa makini hatari zilizokuwepo na kuandaa mpango maalum wa matibabu kabla ya kumfanyia upasuaji. Upasuaji huo ulifanikiwa, Bi Ashfaina alipona kabisa na hatimaye kuruhusiwa kutoka hospitali.
Madaktari hao wa China wamesema kufanikiwa kwa matibabu ya tatizo la Ashfaina kumeziba pengo kubwa la huko kwenye nyanja ya utambuzi na matibabu ya ugonjwa mkubwa na wenye utatanishi wa masikio.

Picha hii inamwonesha Daktari Li Li wa timu ya 35 ya madaktari wa China visiwani Zanzibar, akimsafisha kidonda Ashfaina Omari Ali wadini Zanzibar Tarehe 4 Agosti 2026. (Kikundi cha 35 cha Madaktari wa China Zanzibar/Picha imetolewa na Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



