Lugha Nyingine
Kiongozi wa kundi la Houthi akanusha kuulenga mji wa Makka wakati hali ya wasiwasi ya Saudi Arabia ikiendelea
Kiongozi wa kundi la Houthi nchini Yemen Bw. Abdul-Malik al-Houthi, siku ya Alhamisi alikanusha madai kwamba kundi lake lilijaribu kuushambulia mji mtakatifu wa Kiislamu wa Makka, na kusema madai hayo ni "uzushi na upotoshaji" huku uhasama na Saudi Arabia ukizidi kuongezeka.
Kwenye hotuba aliyotoa kupitia televisheni ya al-Masirah inayomilikiwa na kundi la Houthi, Bw. Al-Houthi amesema madai kuwa vikosi vya kundi lake vinaulenga mji wa Makka ni "uongo," akidai kuwa tuhuma hizo zinalenga kutafuta uungwaji mkono mpana zaidi kwa kile alichokiita "hatua za kijeshi zilizopangwa dhidi ya Yemen."
Bw. Al-Houthi pia ameishutumu Saudi Arabia kwa kushindwa kuendeleza suluhu ya kisiasa wakati wa kipindi cha utulivu kiasi, kabla ya hali ya uhasama kuongezeka hivi karibuni.
Badala yake amesema vizuizi dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Houthi nchini Yemen viliongezwa, vikiwa ni pamoja na vizuizi kwa uendeshaji wa viwanja vya ndege na uingizaji wa bidhaa, hatua hizo ambazo bado ni masuala muhimu ambayo hayajatatuliwa.
Bw. Al-Houthi pia amewataka wafuasi wake kote Yemen kufanya maandamano makubwa siku ya Ijumaa ili kupinga kile alichokiita "uzushi na shutuma za uongo" za Saudi Arabia.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



