Lugha Nyingine
Wahouthi wadai kutungua droni ya Saudi Arabia ya kufanya upelelezi huko Marib, Yemen
Kundi la Houthi nchini Yemen limesema limeitungua droni yenye silaha ya Saudi Arabia inayotumika kwa upelelezi katika jimbo la Marib, kaskazini-mashariki mwa Yemen, na pia kuzuia ndege za kivita za Saudi Arabia katika eneo la pwani ya magharibi mwa nchi hiyo.
Msemaji wa kundi la Houthi, Bw. Yahya Sarea, alisema Jumatano jioni katika taarifa iliyotolewa kupitia kituo cha televisheni cha al-Masirah kinachoendeshwa na kundi hilo, kuwa vikosi vya kundi hilo "muda mfupi uliopita vilitungua droni yenye silaha na inayotumika kwa upelelezi inayomilikiwa na adui wa Saudi Arabia, wakati ikifanya operesheni za uhasama juu ya jimbo la Marib, kwa kutumia silaha za kufaa."
Bw. Sarea amesema katika tukio jingine linalohusiana na hilo, lilitokea saa 12:40 jioni kwa saa za eneo hilo, wakati vikosi vya kundi hilo vilizuia vikundi viwili vya ndege za kivita aina ya F-15 za Saudi Arabia ambazo zilikuwa zimeondoka katika kambi ya jeshi la anga ya Khamis Mushait, kusini-magharibi mwa Saudi Arabia, na kuingia katika anga ya eneo la Mocha katika jimbo la Taiz, magharibi mwa Yemen.
Mapema Jumatano, kundi la Houthi pia liliishutumu Saudi Arabia kwa kufanya mashambulizi zaidi ya 450 katika majimbo saba ya Yemen katika kipindi cha wiki iliyopita.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



