Lugha Nyingine
Kupamba moto kwa vita nchini Yemen kunahatarisha mgogoro mpana zaidi wa kikanda wenye athari duniani: Mjumbe wa UN
UMOJA WA MATAIFA - Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Hans Grundberg, ameonya jana Alhamisi kuwa vita vilivyoanza upya nchini Yemen vinahatarisha kuiingiza nchi hiyo katika mzozo mpana zaidi wa kikanda ambao bado haujatatuliwa, wenye athari duniani.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Usalama la UN jijini New York kwa njia ya video Grundberg amesema katika saa 24 zilizopita, mapigano yameongezeka kwenye maeneo mbalimbali ya mapambano nchini Yemen, hasa kwenye pwani ya kimkakati ya magharibi. Amesema Wahouthi wameanzisha mashambulizi makubwa, ikiwemo dhidi ya Mokha, mji wa bandari ulioko takriban kilomita 75 kutoka Bab al-Mandeb—mlango muhimu wa baharini unaounganisha Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden, ambako sehemu kubwa ya biashara na nishati duniani hupita.
"Hadi kufikia sasa, wamechukua udhibiti wa Mokha, jambo linalowawezesha kudhibiti moja kwa moja njia zinazoelekea kwenye moja ya njia muhimu zaidi za baharini duniani, ingawa mapigano yanaendelea na hali bado ni tete," amesema kupitia njia ya video, "Hali hii inazua wasiwasi mkubwa miongoni mwa jamii ya kimataifa kuhusu tishio kwa uhuru wa usafiri wa majini."
Amesema kuanza upya huko kwa vita moja kwa moja kunaashiria mwisho wa utulivu wa kiasi ambao Yemen imekuwa nao kwa zaidi ya miaka minne tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliyofikiwa kwa upatanishi wa UN. Amesema, vita hivyo si tu kwamba vinatishia kuitumbukiza Yemen katika vita vya muda mrefu na vinavyozidi kupanuka, bali pia vinahatarisha kuiingiza nchi hiyo katika mzozo mpana zaidi wa kikanda ambao haujatatuliwa, wenye athari duniani.
Grundberg ametoa wito kwa Wahouthi kusimamisha mashambulizi ndani ya Yemen na yale ya kuvuka mpaka na kuingia Saudi Arabia, na kusimamisha mashambulizi na vitisho dhidi ya meli za kibiashara.
Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa ameziomba pande zote kuendelea na njia za mawasiliano na kudumisha mchakato kuelekea suluhu ya kisiasa.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



