Lugha Nyingine
China yabonyeza “kitufe cha kutuliza hali”, ikionyesha maono ya kimkakati ya nchi kubwa
Video yenye kichwa “Namna China Kimyakimya Ilivyookoa Dunia” (How China quietly saved the world) – sehemu ya mfululizo wa video za kimataifa kuhusu nishati za mwandishi wa zamani wa safu wa gazeti la The New York Times la Marekani, Max Fisher, hivi karibuni imezua mwitikio mkubwa katika mitandao ya kijamii duniani. Katika video hiyo, Fisher alikunjua ramani ya njia za meli za mafuta duniani na kusema: “Jambo la kushangaza zaidi si nani anagombania mafuta, bali nani anayepunguza hali hiyo.” Video hiyo imepata watazamaji zaidi ya milioni 6.
Ikiwa njia muhimu ya usafirishaji wa nishati duniani, Mlango-Bahari wa Hormuz hivi karibuni umeshuhudia mivutano inayoendelea kuhusu usafiri wa meli, jambo ambalo limepandisha hatari kwenye mafuta ghafi duniani.
Kwa mantiki ya soko ya kawaida, wakati migogoro ya siasa za kijiografia inaposababisha hofu ya ugavi, nchi walaji wakubwa mara nyingi huharakisha manunuzi na kulimbikiza akiba, na matokeo ya kuongezeka kwa pengo la mahitaji na ugavi huzidi kusukuma bei ya mafuta juu, hivyo kusababisha mfumuko wa bei duniani kupitia kuongezeka kwa gharama za nishati.
Baada ya kupamba moto hivi karibuni kwa mivutano katika Mashariki ya Kati, hofu ya soko kwamba kurudi juu kwa bei za nishati kutaathiri ufufuaji wa uchumi duniani iliendelea kuongezeka, na matarajio ya “kugombania mafuta” yalienea kwa muda mfupi katika soko la biashara ya bidhaa ghafi.
Hata hivyo, soko la China limetoa jibu tofauti. Kampuni za kuchakata mafuta na za kemikali za China zilirekebisha ratiba zao za uzalishaji kulingana na hali halisi, kwa unyumbulifu na utaratibu zilipunguza kasi ya manunuzi mapya ya mafuta ghafi yenye bei ya juu, hivyo kutuliza kasi ya kuongezeka kwa uagizaji wa mafuta kwa upande wa mahitaji.
Kwa namna ya kujizuia sana, China kwa ufanisi ilibonyeza “kitufe cha kutuliza hali” kwa uwiano wenye shinikizo wa ugavi na mahitaji duniani.
Makala kwenye Jarida la Wall Street imebainisha kwamba hatua hiyo ya China ya kupunguza uagizaji wa mafuta imetoa uungaji mkono muhimu kwa uchumi duniani uliokuwa chini ya shinikizo; gazeti la Ufaransa Le Figaro limeandika kwamba hii ni mara ya pili tangu kutokea msukosuko wa kifedha wa kimataifa wa 2008 kwamba China imechukua jukumu muhimu katika kutuliza uchumi wa dunia.
Kwa muda mrefu, mikakati duniani kwa ajili ya kukabiliana na misukosuko ya mafuta ililenga zaidi upande wa ugavi, ikiziacha nchi walaji wakubwa kwa kiasi kikubwa zikibeba mabadiliko ya bei bila kuwepo kwa hatua stahiki. Hata hivyo, uzoefu wa hivi karibuni umeonyesha kwamba masoko ya walaji wakubwa mno yanaweza pia kufanya kazi ya kuwa watuliza hali - kupitia kurekebisha uwezo wa uzalishaji na usimamizi wa akiba - hivyo kuwa nguvu muhimu katika kudumisha uwiano wa soko.
Shirika la Habari la Reuters limeandika kwamba upunguzaji wa China wa manunuzi ya mafuta ghafi tangu kupamba moto kwa hivi punde zaidi kwa mivutano katika Mashariki ya Kati, kwa kiasi kikubwa, kumepunguza athari zilizosababishwa na mabadiliko ya ugavi katika Mashariki ya Kati; Gazeti la Financial Times pia limetoa maoni kwamba China inaibuka kuwa upande muhimu unaotoa mchango kwenye uwiano wa soko la mafuta duniani.
Ni kwa namna gani China imeweza kubadili mwelekeo na kufuata njia tofauti? Kujiamini huku kunatokana na maono ya kimkakati ya China.
Wakati wa kipindi cha bei ya chini ya mafuta kimataifa miaka michache iliyopita, China ilisukuma kwa utulivu ujenzi wa mfumo wa akiba wa kibiashara, hatua kwa hatua ikijenga akiba kubwa. Katikati ya kupanda kwa bei ya mafuta kwa hivi karibuni, soko la ndani ya China lilikuwa limesimamisha mwenendo wake wa kawaida wa kuongeza akiba ya kibiashara, na badala yake ilichagua kutumia ipasavyo akiba iliyokuwepo kuwa mbadala wa sehemu ya bidhaa za kuagizwa nje zenye bei ya juu.
Kupitia kufanya kazi bila kukoma na kwa kina, China imeunda mfumo mzuri na wenye ufanisi wa mzunguko wa akiba ya kibiashara; vyanzo vya uagizaji wa mafuta ghafi vinaendelea kupanuka kwa nchi na maeneo kama vile Brazil na Afrika na maeneo mengine duniani, hivyo kupunguza hatua kwa hatua utegemezi wa njia yoyote moja ya usafirishaji.
Takwimu za Shirika la Kimataifa la Nishati zinaonyesha kwamba katika robo ya pili ya mwaka huu, magari yanayotumia umeme pekee yalikua mbadala wa matumizi ya wastani wa mapipa milioni 1.5 ya mafuta ghafi kwa siku nchini China, kiasi ambacho kilizidi kwa mbali matarajio ya awali ya soko ya watu wengi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



