Wachambuzi wa Afrika watoa wito wa kuzidisha uhusiano na China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 09, 2026

Kreni ikiinua kontena katika Stesheni ya Port Reitz kwenye Reli ya SGR ya Mombasa-Nairobi (SGR), Mombasa, Kenya, Julai 9, 2026. (Xinhua/Xie Jianfei)

Kreni ikiinua kontena katika Stesheni ya Port Reitz kwenye Reli ya SGR ya Mombasa-Nairobi (SGR), Mombasa, Kenya, Julai 9, 2026. (Xinhua/Xie Jianfei)

NAIROBI - Afrika lazima iimarishe ushirikiano wa kimkakati, hasa na nchi kama China, ili kufungua uwekezaji katika miundombinu, teknolojia ya kidijitali na ufikiaji wa masoko mapya, wachambuzi wamebainisha.

Onyango K'Onyango, mtaalamu Mkenya wa uhusiano kati ya China na Afrika, amesisitiza kwamba bara hilo linahitaji uwekezaji wa kiwango-kikubwa kwa haraka katika mitandao ya usafiri, mifumo ya umeme, teknolojia ya kidijitali, utengenezaji bidhaa, na rasilimali watu.

"Mahitaji haya hayawezi kutimizwa kupitia rasilimali za ndani pekee. Afrika, kwa hiyo, inahitaji ushirikiano wa kimataifa ambao unatoa mtaji, teknolojia, masoko na utaalamu huku ikiunga mkono vipaumbele vyake yenyewe vya maendeleo," amesema.

K'Onyango amejenga hoja kwamba mwelekeo wa kivitendo wa China unachochea ushirikiano wa kiuchumi wenye maana barani Afrika, akibainisha kuwa miradi ya miundombinu iliyofadhiliwa na taifa hilo la Asia imeongeza muunganisho wa kikanda na kupanua fursa za biashara kote barani humo.

"Reli, barabara kuu, bandari na vituo vya nishati si miundo ya kuonekana kihalisia tu; vinapunguza gharama ya kusafirisha bidhaa, kuunganisha wazalishaji na masoko na kuimarisha mafungamano ya kiuchumi ya kikanda," amesema.

Mwanamke akichanganua parachichi shambani mwake katika Kaunti ya Nakuru, Kenya, Juni 16, 2026. (Picha na Sheikh Maina/Xinhua)

Mwanamke akichanganua parachichi shambani mwake katika Kaunti ya Nakuru, Kenya, Juni 16, 2026. (Picha na Sheikh Maina/Xinhua)

Lee Kinyanjui, waziri wa uwekezaji, biashara na viwanda wa Kenya, amebainisha kuwa sera ya China ya ushuru-sifuri itafungua uwezekano mkubwa kwa wauzaji nje wa Kenya, hasa katika kilimo, na kusaidia kulifanya kapu la mauzo ya nje kuwa la bidhaa mbalimbali.

Kinyanjui amesema katika taarifa ya hivi karibuni kwamba mageuzi ya haraka ya kiviwanda ya China, ukuaji wa miundombinu, na upigaji hatua kiteknolojia vinatoa masomo muhimu kwa nchi za Afrika kubadilika kuendana na mazingira halisi ya ndani.

Naye msomi wa uhusiano wa kimataifa Macharia Munene amebainisha katika maoni ya hivi karibuni kwamba Afrika lazima itoe kipaumbele kwa biashara yenye usawa, uhamishaji teknolojia, na ujengaji uwezo wa viwanda wa ndani.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha