Xi Jinping afanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Uingereza

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 09, 2026

BEIJING - Rais wa China Xi Jinping amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Uingereza Andy Burnham jana Jumanne ambapo amempongeza Burnham kwa kupewa wadhifa wa waziri mkuu wa Uingereza, na amesema China na Uingereza ni washirika wa kimkakati wa pande zote.

Amesema ingawa nchi zetu mbili zina tofauti katika mifumo ya jamii na hali ya nchi, lakini maslahi yao ya pamoja ni zaidi kuliko hali ya tofauti. Xi ametoa wito wa kutaka pande hizo mbili kuheshimiana na kuaminiana, kuzishinda tofauti, kutafuta maoni ya pamoja na kuweka tofauti kando, na kupanua ushirikiano wa kunufaishana.

Amesema serikali za nchi mbili zote zimefanya juhudi kubwa za kuendeleza uchumi wao na kuboresha maisha ya watu, na nchi hizo mbili pia zinaweza kusaidiana kwa nguvu bora za kila upande na kusukuma mbele maendeleo ya kila moja kati ya nchi hizo mbili.

Amesema wakati wa kipindi cha Mpango wa 15 wa Miaka Mitano (2026-2030), China itapanua zaidi ufunguaji mlango katika sekta za elimu, matibabu na afya na mambo ya fedha, ambazo zote hizo zitatoa uwezekano mkubwa kwa ushirikiano wa pande mbili.

Xi amesema, China na Uingereza zote ni nchi kubwa katika sayansi na teknolojia, na zina rasilimali nyingi katika sekta za elimu, utamaduni, na michezo. Ametoa wito wa kutaka pande hizo mbili kuwa na msimamo wa kufungulia mlango na kutupia macho siku za baadaye, na kuimarisha mawasiliano na ushirikiano katika sekta mbalimbali.

Xi amedhihirisha kuwa China na Uingereza, zikiwa nchi wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na zenye uchumi mkubwa duniani, zote zinaunga mkono ushirikiano wa pande nyingi na biashara huria na zinashikilia umuhimu wa kiini wa Umoja wa Mataifa.

Amesema pande hizo mbili zinapaswa kuimarisha mawasiliano na uratibu ndani ya mifumo ya Umoja wa Mataifa, Kundi la nchi 20 na Shirika la Biashara Duniani, na kuhimiza dunia ya ncha nyingi yenye usawa na utaratibu na utandawazi wa uchumi wa dunia wenye manufaa na jumuishi kwa wote.

Kwa upande wake Burnham amesema Uingereza inapenda kudumisha sera yake iliyopo kuhusu China na itajikita kithabiti katika kuendeleza uhusiano wa washirika wa kimkakati wa muda mrefu na tulivu kati ya Uingereza na China.

Burnham amesema, Uingereza inashikilia msimamo wake juu ya suala la Taiwan. Ameongeza kuwa katika hali ya kimataifa yenye misukosuko na utatanishi, na inayobadilika badilika, Uingereza na China zikiwa nchi wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zinapaswa kuhimiza utatuzi wa matatizo makubwa ya kimataifa kwa kupitia mazungumzo, kukabiliana kwa pamoja na changamoto zinazoikumba dunia nzima kama vile mabadiliko ya tabianchi, na kushirikiana katika kulinda utulivu na ustawi wa dunia.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha