Rais wa zamani wa Sierra Leone arudi nyumbani baada ya kufutiwa mashtaka ya uhaini

(CRI Online) Septemba 08, 2026

Rais wa zamani wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma amerudi Freetown, mji mkuu wa nchi hiyo, Jumapili baada ya kufutiwa mashtaka ya jinai dhidi yake yanayohusiana na jaribo la kupindua serikali.

Serikali ya Sierra Leone ilifuta mashtaka ya jinai dhidi ya rais huyo wa zamani mwezi Julai, ikimaliza kesi ya kisheria kutokana na jaribio lililoshindwa la mapinduzi la mwezi Novemba mwaka 2023.

Koroma alishitakiwa kwa uhaini na kuwekwa kizuizini nyumbani kwake baada ya wanajeshi wenye silaha kushambulia kambi ya kijeshi na gereza mbili mjini Freetown, na kuwaachia huru wafungwa zaidi ya 2,200. Watu zaidi ya 21 wakiwemo wanajeshi 14 waliuawa katika mapigano wakati wa tukio hilo.

Serikali ilidai kuwa washambuliaji waliungwa mkono na rais huyu wa zamani, lakini Koroma alikanusha.

Rais huyo wa zamani aliyekuwa madarakani kutoka mwaka 2007 hadi 2018, alipewa dhamana kwa sababu za kiafya na kuruhusiwa kwenda Nigeria mwezi Januari 2024.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha