AU yakaribisha upitishaji wa UN wa ramani ambazo zinaonyesha ukubwa sahihi wa Afrika

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 07, 2026

Picha hii iliyopigwa Februari 11, 2026 ikionyesha makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa, Ethiopia. (Xinhua/Xie Jianfei)

Picha hii iliyopigwa Februari 11, 2026 ikionyesha makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU), Addis Ababa, Ethiopia. (Xinhua/Xie Jianfei)

ADDIS ABABA - Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Mahmoud Ali Youssouf, amekaribisha azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa linalohimiza matumizi ya makadirio ya ramani ya Dunia yenye Ukubwa Sawa (Equal Earth) kwenye ramani duniani kote ili kuwa mbadala wa makadirio ya ramani ya Mercator yanayotumika zaidi hadi sasa, ambayo yanapotosha ukubwa wa ardhi ya bara hilo.

Kwenye taarifa iliyotolewa Ijumaa, Youssouf amepongeza uongozi wa Jamhuri ya Togo, ambao umesimamia mpango huo kwa niaba ya Afrika na kusaidia kuhamasisha uungwaji mkono mpana ndani ya jumuiya ya kimataifa. Pia amezipongeza nchi wanachama wa AU kwa umoja wao na uhamasishaji wa pamoja katika kuunga mkono mpango huo.

AU imesema kupitishwa kwa azimio hilo ni mwanzo wa hatua muhimu kwenda mbele. Imesema, makadirio hayo ya ramani ya Mercator yaliyoundwa katika karne ya 16 hasa kwa ajili ya usafiri majini, hayaakisi kwa usahihi maeneo ya ardhi ya maeneo tofauti ya dunia na kwa kiasi kikubwa yanapunguza ukubwa halisi wa bara la Afrika.

Taarifa hiyo ya AU imsema zaidi ya makadirio hayo ya ramani, mpango huo unasisitiza umuhimu wa kuiwakilisha Afrika kwa msingi wa ukweli halisi na uliothibitishwa kisayansi. Imesema, katika suala hilo, mwenyekiti amehimiza taasisi za kimataifa, mifumo ya elimu, wachapishaji na majukwaa ya kidijitali kuhimiza hatua kwa hatua matumizi ya uwakilishi wa makadirio ya ramani unaoakisi kwa usahihi zaidi maeneo halisi ya ardhi.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipiga kura siku ya Ijumaa kupitisha azimio hilo lisilolazimisha kisheria ambalo linahimiza matumizi ya makadirio ya ramani ya Dunia yenye Ukubwa Sawa kwenye ramani duniani kote ili kuwa mbadala wa makadirio ya Mercator.

Azimio hilo la 'Sahihisha Ramani', linalolenga kusawazisha uwakilishi wa ramani duniani na kuhimiza uwakilishi wenye ukubwa sawa wa maeneo ya dunia, hasa Afrika, lilipitishwa kwa kura 164 zilizounga mkono, 1 ya kupinga, na 6 zilizojizuia.

Linatambua kwamba makadirio ya ramani ya Mercator, yanayotumika sana kote duniani, yanapotosha ukubwa wa ardhi ya bara ulio mbali na ikweta, hali ambayo inasababisha kupungua kwa uwiano wa ukubwa wa Afrika na maeneo mengine.

Mahmoud Ali Youssouf, mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), akihutubia Mkutano wa 49 wa Kawaida wa Baraza la Utendaji la AU, Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, Julai 28, 2026. (Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika/kupitia Xinhua)

Mahmoud Ali Youssouf, mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), akihutubia Mkutano wa 49 wa Kawaida wa Baraza la Utendaji la AU, Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, Julai 28, 2026. (Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika/kupitia Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha