Iran kutangaza "eneo la kuzuiliwa" nje ya Mlango-Bahari wa Hormuz

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Septemba 07, 2026

Picha hii iliyopigwa Juni 20, 2026 ikionyesha Mlango-Bahari wa Hormuz karibu na Khasab, mji mdogo kaskazini mwa Oman. (Xinhua/Wen Xinnian)

Picha hii iliyopigwa Juni 20, 2026 ikionyesha Mlango-Bahari wa Hormuz karibu na Khasab, mji mdogo kaskazini mwa Oman. (Xinhua/Wen Xinnian)

TEHRAN - Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran Mohsen Rezaei amesema kwamba nchi yake itatangaza eneo la kuzuiliwa nje ya Mlango-Bahari wa Hormuz katika siku zijazo na kuweka meli yoyote inayojaribu kupita kwenye eneo hilo katika orodha ya vikwazo vya Tehran.

Kwenye mahojiano na Televisheni ya IRIB inayoendeshwa na serikali ya Iran, ambayo yamerushwa jana Jumapili usiku, Rezaei amesema kwamba eneo hilo litaenea kutoka "mstari ambapo kizuizi cha majini cha Marekani kinaanzia hadi eneo la Mlango-Bahari wa Hormuz na ndani ya Ghuba ya Uajemi iliyopo upande mwingine (wa mlango-bahari huo)."

Meli zinazoingia kwenye eneo hilo bila uratibu na Iran, ameongeza, zitakabiliwa na vikwazo vinavyoathiri bima yao na upitaji wao wa baadaye kupitia njia hiyo ya maji.

Rezaei ameielezea hatua hiyo kuwa ni sehemu ya mabadiliko mapana zaidi ya kimkakati katika mbinu ya Iran ya vita na diplomasia, ikilenga kuongeza shinikizo kwa Washington.

Afisa huyo wa usalama amesisitiza kwamba Mlango-Bahari wa Hormuz umefungwa kabisa, akipinga madai ya Marekani kwamba meli na meli za mafuta zinavuka njia hiyo ya maji akiyaita kuwa ni "uongo."

Huku akikiri kwamba baadhi ya meli hujaribu kuvuka mlango-bahari huo kupitia njia karibu na Oman, mara nyingi zikizima mifumo yao ya urambazaji ili kukwepa kubainiwa, Rezaei amesema meli nyingi kati ya hizo "hupokea vipigo."

Lakini ameongeza kwamba Iran haikusudii kuzizamisha kwa sasa kutokana na wasiwasi wa kimazingira.

Rezaei ametangaza zaidi kwamba Iran imejaribu kurusha kwa mara ya kwanza kombora la kuharibu manowari lililotengenezwa na Iran yenyewe ndani ya nchi juu ya manowari ya Marekani ya kubeba ndege ndani saa 48 zilizopita, akiielezea hatua hiyo kuwa ni onyo kwamba kizuizi hicho cha majini cha Marekani ni dhaifu.

Rezaei amesema Mlango-Bahari wa Hormuz utaendelea kufungwa isipokuwa pale Marekani itakapochukua hatua za kivitendo kutimiza majukumu yake chini ya nyaraka ya makubaliano ya amani iliyosainiwa kati ya Tehran na Washington mwezi Juni.

Kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran Februari 28, Tehran ilizuia upitaji kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz, wakati huohuo vikosi vya Marekani vimeweka kizuizi cha majini kinacholenga meli zinazosafiri kwenda au kutoka bandari za Iran na maeneo ya pwani.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha