Lugha Nyingine
IRGC ya Iran yasema watu kadhaa wameuawa katika shambulio la Marekani kwenye Kisiwa cha Larak, yajibu mapigo
TEHRAN - Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran (IRGC) kimesema wanajeshi na raia kadhaa wameuawa au kujeruhiwa jana Jumapili usiku katika shambulio la "Marekani na Israeli" kwenye Kisiwa cha Larak kusini mwa Iran katika Jimbo la Hormozgan na imetoa taarifa mapema leo Jumatatu kwamba imejibu mapigo dhidi ya shambulio hilo.
Likirejelea ripoti zisizo rasmi, shirika la habari la Tasnim la Iran limesema kwamba angalau watu wawili wameuawa na wengine wawili wamejeruhiwa katika kile kilichoelezwa kuwa ni "shambulio la droni" la Marekani kwenye kisiwa hicho.
CNN, ikimrejelea afisa wa Marekani, imeripoti kuwa jeshi la Marekani jana Jumapili lilishambulia kisiwa hicho baada ya kuona vikosi vya Iran "vikijiandaa kurusha mabomu ya majini kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz."
Wakati huohuo IRGC imesema katika taarifa yake leo Jumatatu kwamba vikosi vyake vya anga vimefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa droni na makombora ya balestiki dhidi ya maeneo lengwa ya Marekani kwenye kambi mbili za jeshi la anga nchini Jordan mapema leo.
Mashambulizi hayo yalikuwa ni kujibu "mashambulizi ya anga ya Marekani na Israeli" dhidi ya Kisiwa cha Larak kusini mwa Iran katika Jimbo la Hormozgan Jumapili usiku, IRGC imesema katika taarifa yake iliyochapishwa na chombo chake rasmi cha habari, Sepah News.
Taarifa hiyo imebainisha kambi za jeshi la anga zilizolengwa kuwa ni za Mfalme Hussein na Al-Azraq, ikisema kwamba mashambulizi hayo yamepiga miundombinu ya kiufundi na ya matengenezo vilevile hangari za ndege za kivita za Marekani, na kusababisha uharibifu mkubwa.
IRGC imesema shambulio hilo ni "adhabu kwa mchokozi," ikibainisha kwamba "mashambulizi na uhalifu havitatatua shauku kubwa ya adui kudhoofisha udhibiti wa Iran juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz."
Imeongeza kuwa kila hatua ya kijeshi itakayochukuliwa na "adui" itakabiliwa na majibu "mabaya" zaidi.
Mashambulizi hayo ni ya kwanza ya Marekani dhidi ya maeneo lengwa ya Iran katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



