Lugha Nyingine
Xi kuhudhuria mkutano wa viongozi wa SCO na kufanya ziara ya kiserikali nchini Kyrgyzstan na Misri
BEIJING - Wizara ya mambo ya nje ya China imetangaza jana Jumatano kwamba kuanzia Agosti 30 hadi Septemba 3, Rais wa China Xi Jinping atahudhuria Mkutano wa Viongozi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) 2026 mjini Bishkek, na kufanya ziara ya kiserikali nchini Kyrgyzstan na Misri kutokana na mwaliko wa Rais Sadyr Japarov wa Kyrgyzstan na Rais Abdel Fattah El-Sisi wa Misri.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari alipoulizwa habari zaidi kuhusu safari hiyo, msemaji wa wizara hiyo Lin Jian amesema, mwaka huu ni wa maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa SCO. Amesema, kwenye Mkutano huo wa Bishkek, Xi atabadilishana maoni kwa kina na viongozi washiriki kuhusu kuzidisha ushirikiano wa SCO katika sekta mbalimbali chini ya hali mpya na masuala makubwa ya kimataifa na kikanda.
Lin amesema watatoa mwelekezo kwa maendeleo yenye sifa bora ya SCO na ushiriki wake katika mageuzi na maendeleo ya mfumo wa usimamizi wa dunia nzima.
Lin amesema, wakati wa ziara yake ya Kyrgyzstan, Xi atabadilishana maoni kwa kina na kiongozi wa Kyrgyzstan kuhusu uhusiano wa pande mbili, ushirikiano katika maeneo muhimu, na hali ya kimataifa na kikanda, na pia atashiriki kwenye shughuli mbalimbali za kiserikali.
Lin amesema China inatarajia kufanya ushirikiano na Kyrgyzstan, na kuchukua ziara hiyo kama fursa ya kuhimiza maendeleo yenye sifa bora ya ushirikiano wa kunufaishana, kuongeza mambo mapya kwenye jumuiya ya China na Kyrgyzstan yenye mustakabali wa pamoja, na kuleta manufaa zaidi kwa watu wa nchi hizo mbili.
Msemaji huyo amesema, ziara ya Xi nchini Misri, ambayo ni ziara yake ya kwanza ya kiserikali nchini humo katika muongo mmoja, itafanyika wakati wa maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia wa China na Misri.
Lin amesema marais wa China na Misri watabadilishana maoni kwa kina kuhusu uhusiano wa nchi mbili na masuala ya kimataifa na kikanda yanayofuatiliwa na pande zote mbili.
Lin ameongeza kuwa kwa kupitia ziara hiyo, China inatarajia kushirikiana na Misri katika kuendeleza urafiki wa jadi, kupeana uungaji mkono thabiti, kupanua ushirikiano wa kunufaishana, na kuimarisha ujenzi wa mambo ya kisasa wa kila upande, na hivyo kwa pamoja kuandika ukurasa mpya wa uhusiano wa pande mbili na kutoa mchango kwa ajili ya amani na utulivu wa kikanda na duniani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



