Watu 12,700 wahamishwa kutokana na mvua kubwa kunyesha Liaoning kaskazini-mashariki mwa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Agosti 25, 2026

Barabara iliyofurika maji mengi ikionekana Shenyang mkoani Liaoning, kaskazini-mashariki mwa China, Agosti 24, 2026. (Xinhua/Li Gang)

Barabara iliyofurika maji mengi ikionekana Shenyang mkoani Liaoning, kaskazini-mashariki mwa China, Agosti 24, 2026. (Xinhua/Li Gang)

SHENYANG - Serikali ya mtaa ya mkoa wa Liaoning imesema kuwa, hadi jana Jumatatu asubuhi watu wapatao 12,700 walikuwa wamehamishwa kwenye sehemu mbalimbali zenye usalama mkoani humo kutokana na mvua kubwa kunyesha katika mkoa huo tangu Jumapili asubuhi.

Mvua kubwa hadi ya kiwango cha kupitiliza ilinyesha kusini-mashariki mwa mkoa huo wa Liaoning kuanzia saa 2 asubuhi ya Jumapili iliyopita hadi saa 5 ya asubuhi ya jana Jumatatu, huku mvua kubwa za ghafla zikinyesha katika baadhi ya maeneo. Wakati huohuo sehemu za kaskazini na magharibi mwa mkoa huo zilishuhudia mvua ndogo au ya ukubwa wa kati, na sehemu chache tu zilikumbwa na mvua kubwa, au mvua ya kiwango cha kupitiliza.

Lakini sehemu mbalimbali mkoani Liaoning zilikuwa zimetoa tahadhari nyekundu za mvua ya kiwango cha kupitiliza. Na makao makuu ya kuzuia mafuriko na kupambana na ukame ya mkoa huo ilisema kuwa ilipofikia saa 12 asubuhi jana Jumatatu, miji tisa ilikuwa imeanzisha mwitikio wa kukabiliana na dharura ya mafuriko.

Idara ya kukabiliana na dharura ya mkoa huo imeagiza miji minane, ikiwa ni pamoja na Dalian, Anshan na Dandong, kuweka timu 3,611 za uokoaji na mwitikio wa kukabiliana na dharura zenye jumla ya watu 127,000 katika hali ya utayari kwa ajili ya kupambana na mafuriko. Mji wa Dandong pekee ulikuwa umehamisha watu 8,078 hadi saa 12 asubuhi jana Jumatatu.

Kituo cha hali ya hewa cha Dandong kilitoa tahadhari nyekundu juu ya mvua ya kiwango cha kupitiliza saa 5:33 asubuhi jana Jumatatu, kikiripoti kwamba mvua ya 160 hadi 240 mm ilikuwa imenyesha kwenye eneo la mjini katika muda wa saa 11 zilizopita.

Kituo hicho kimekadiria kuwa, mvua nyingine ya 100 hadi 130 mm itanyesha kuanzia saa sita hadi saa nane zijazo, ambapo kiwango cha juu cha mvua kwa saa kitafikia 70 mm na mfululizo wake wa jumla huenda utazidi 350 mm ifikapo mwisho wa unyeshaji wa mvua hiyo.

China imekuwa na mfumo wa kutoa tahadhari ya hali ya hewa wa ngazi nne, tahadhari nyekundu ikiwakilisha tahadhari kali zaidi, ikifuatiwa na rangi ya chungwa, njano na bluu.

Picha iliyopigwa Agosti 24, 2026 ikionyesha Mto Hunhe wa Mji Shenyang mkoani Liaoning, kaskazini mashariki mwa China. (Xinhua/Li Gang)

Picha iliyopigwa Agosti 24, 2026 ikionyesha Mto Hunhe wa Mji Shenyang mkoani Liaoning, kaskazini mashariki mwa China. (Xinhua/Li Gang)

Magari yakipita kwenye barabara iliyofurika maji huko Shenyang  mkoani Liaoning, kaskazini mashariki mwa China, Agosti 24, 2026. (Xinhua/Li Gang)

Magari yakipita kwenye barabara iliyofurika maji huko Shenyang mkoani Liaoning, kaskazini mashariki mwa China, Agosti 24, 2026. (Xinhua/Li Gang)

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha