Lugha Nyingine
Marekani Yatishia Vikwazo vya "D-Day ya Uchumi" Dhidi ya Iran

Picha hii iliyopigwa Agosti 24, 2026 ikionyesha Wizara ya Fedha ya Marekani, Washington, D.C., Marekani. (Xinhua/Li Rui)
NEW YORK - Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent ameitishia Iran kwa "D-Day ya Uchumi," akitangaza wimbi la vikwazo vipya vinavyolenga kuitenga zaidi nchi hiyo.
"Tunaanzisha mashambulizi makali ya kiuchumi dhidi ya mahusiano ya kifedha ya Iran kote duniani," amesema Bessent jana Jumatatu kwenye mkutano na waandishi wa habari. "Lengo letu ni kukata kila njia ya uhai ya kiuchumi" ambayo inategemewa na nchi hiyo.
Wizara ya Fedha ya Marekani imesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba maamuzi hayo mapya ya vikwazo vya kisekta yanalenga sekta tano muhimu -- mali za kidijitali, teknolojia, dhahabu, usafiri wa anga na usafirishaji wa meli -- ambazo Marekani inasema Iran imekuwa ikizitegemea ili kuunga mkono uchumi wake.
Wizara hiyo inapanua aina za "mambo yanayohusiana na Iran" ambayo Marekani inaweza kuyawekea vikwazo katika siku zijazo, na ikasema "kila nchi itapewa muda maalum wa kufunga shughuli zinazohusiana na Iran" ambazo Marekani imezibainisha.
Bessent amebainisha kwamba Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa akiwapigia simu viongozi duniani akiwaomba mahsusi kukomesha maingiliano yao na Iran.
Wakati huo huo, Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) ya wizara hiyo imeziwekea vikwazo taasisi, watu binafsi, na meli karibu 60 katika maeneo ya mamlaka mbalimbali zinazowezesha shughuli za Iran, ikiwemo ununuzi haramu wa teknolojia ya nyuklia na makombora, operesheni za mtandaoni, na mitandao ya kuzalisha mapato ya mafuta.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, Spika wa Bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf amejibu vitisho hivyo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Tehran kwa kusema kwamba, "Washirika wa biashara wa Iran, katika vyombo vya habari na kupitia ujumbe uliotumwa kwetu, wameweka wazi kwamba hawatilii maanani kauli hizi hata kidogo."
"Hawawezi kukata njia zetu za uhai wa kifedha," Waziri wa Mambo ya Uchumi na Fedha wa Iran Seyed Ali Madanizadeh amesema katika ujumbe mwingine kwenye mtandao wa X, akiongeza kwamba Tehran imekuwa "ikipanga kwa muda fulani kukabiliana na vikwazo hivyo."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



