Lugha Nyingine
Mkutano wa mawaziri wa SME wa APEC 2026 kujikita katika uvumbuzi na ushirikiano

Mapambo yanayohusu mkutano wa APEC yakionekana kwenye eneo la biashara, Shenzhen, Mkoa wa Guangdong, kusini mwa China, Agosti 10, 2026. (Xinhua/Liang Xu)
BEIJING - Mkutano wa 32 wa Mawaziri wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia-Pasifiki (APEC) kuhusu Kampuni za Ukubwa Mdogo na wa Kati (SME) utafanyika Septemba 4 mjini Guangzhou, Mkoa wa Guangdong, kusini mwa China, Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Kupashana Habari ya China (MIIT) imetangaza jana Jumatatu.
Mkutano huo, wenye kaulimbiu ya "maendeleo yanayoendeshwa na uvumbuzi kwa ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote," utawakutanisha maafisa wanaoshughulikia mambo ya SME kutoka pande mbalimbali za APEC, wawakilishi wa Sekretarieti ya APEC, na wageni wengine.
Liang Zhifeng, mkurugenzi wa ofisi ya SME chini ya wizara hiyo amesema, mkutano huo utajikita katika uvumbuzi wa kiteknolojia, uwezeshaji wa kidijitali na maendeleo jumuishi, huku taarifa ya pamoja ya mawaziri na nyaraka zingine za matokeo zikitarajiwa.
Naibu Waziri wa Viwanda na Teknolojia ya Kupashana Habari wa China Ke Jixin amesema, kama mwenyeji, China inatumai kwamba kupitia mabadilishano ya kina, pande zote za uchumi zitafikia makubaliano ya kivitendo yanayotazama mbele, kuhimiza kufunzana katika sera na matokeo halisi, na kwa pamoja kuongeza uwezo wa uvumbuzi, kiwango cha mambo ya kidijitali na uwezo wa maendeleo endelevu wa kampuni za ukubwa mdogo na wa kati katika eneo la Asia-Pasifiki.
Wang Sheng, makamu mkuu wa mkoa wa Guangdong, amesema kwamba maandalizi yote ya mkutano huo kimsingi yamekamilika, na pande zote za APEC zimethibitisha ushiriki wao. Amesema, kampuni zaidi ya 2,100 kutoka ndani na nje ya China zimejisajili kwa maonyesho yatakayoambatana na mkutano huo, huku mabanda zaidi ya 3,900 yakiwa yamepangwa.
China itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 33 wa Viongozi wa Uchumi wa APEC mjini Shenzhen kusini mwa China mwezi Novemba mwaka huu, ambayo itakuwa ni mara ya tatu kwa nchi hiyo kuwa mwenyeji wa mkutano huo baada ya Shanghai mwaka 2001 na Beijing mwaka 2014.
Mwaka huu unaadhimisha "Mwaka wa China" wa APEC, wenye kaulimbiu ya "Kujenga Jumuiya ya Asia-Pasifiki Ili Kustawi Pamoja." Mikutano na shughuli takriban 300 zinazohusiana na APEC zitafanyika katika miji mbalimbali ya China mwaka mzima.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



