Lugha Nyingine
Rais wa DRC azindua kiwanda cha maji kilichojengwa na kampuni za China

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi akizindua kiwanda cha maji kilichojengwa na kampuni ya China, Kamina, mji mkuu wa jimbo la kusini la Haut-Lomami la DRC, Julai 29, 2026. (Xinhua)
KINSHASA - Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi amezindua kiwanda cha kutibu maji Jumatano wiki hii kilichojengwa na kampuni za China huko Kamina, mji mkuu wa jimbo la kusini la Haut-Lomami.
Tshisekedi alitembelea sehemu za uendeshaji wa kiwanda hicho, akakagua vifaa vyake vya kutibu maji na pia akatazama sampuli ya maji kabla ya kuwasha rasmi mfumo wa kusukuma maji, huku akielezea kuridhika na mradi huo, kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya DRC.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi, Waziri wa Rasilimali za Maji na Umeme wa DRC Aime Sakombi Molendo amesema mradi huo utasaidia kuboresha hali ya maisha na afya ya umma kwa wakazi wenyeji na utaimarisha uwezo wa kutibu maji ya kunywa wa nchi hiyo.
Balozi wa China nchini DRC Zhao Bin amesema kiwanda hicho cha maji cha Kamina ni mradi ulioanzishwa kupitia ushirikiano wa kivitendo kati ya China na DRC.
Amesema China iko tayari kufanya kazi na DRC ili kuzidisha ushirikiano wa kivitendo katika nyanja mbalimbali na kutoa manufaa zaidi kwa watu wa nchi hizo mbili.
Kiwanda hicho kilichosanifiwa kuwa na uwezo wa kusambaza maji mita za ujazo zaidi ya 7,000 kwa siku, kinatarajiwa kutoa maji ya kunywa yanayokidhi viwango vya afya vya nchi hiyo kwa wakazi wa Kamina na maeneo ya jirani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



