Lugha Nyingine
Andy Burnham awa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, atangaza baraza jipya la mawaziri

Andy Burnham na mkewe wakipungia mkono umati nje ya Mtaa No. 10 wa Downing jijini London, Uingereza, Julai 20, 2026. (Xinhua/Li Ying)
LONDON - Uingereza imeingia katika serikali mpya jana Jumatatu baada ya kiongozi wa chama cha Labour Andy Burnham kuchukua nafasi ya kuwa waziri mkuu mpya na kutangaza baraza lake la mawaziri, akiahidi mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiuchumi.
Burnham amekuwa waziri mkuu wa Uingereza rasmi baada ya Mfalme Charles III kumwalika kuunda serikali katika Kasri la Buckingham. Amechukua nafasi ya Keir Starmer, ambaye hapo awali alikuwa amewasilisha barua ya kujiuzulu kwake kwa Mfalme.
Baadaye Burnham alitoa hotuba yake ya kwanza akiwa waziri mkuu nje ya Mtaa No.10 wa Downing. Huku akisema kuwa yeye ni waziri mkuu wa saba wa Uingereza tangu 2016, amekiri kwamba wanasiasa "hawakuwa wazuri vya kutosha" na akaahidi kufanya bora zaidi.
"Tutafanya wakati huu kuwa wa kufanya mambo mapya kwa Uingereza, na kuleta mabadiliko makubwa zaidi kuwahi kutokea katika miaka 40 iliyopita, mfumo mpya wa siasa na mfumo mpya wa uchumi," amesema.
Burnham amesema serikali yake itafanya siasa kuwa "shirikishi zaidi" na kujikita katika "utatuzi wa matatizo" badala ya "kujipatia pointi za kisiasa."

Andy Burnham akitoa hotuba yake ya kwanza tangu awe waziri mkuu wa Uingereza nje ya Mtaa No. 10 wa Downing jijini London, Uingereza, Julai 20, 2026. (Xinhua/Li Ying)
Saa chache baada ya kuchukua madaraka, Burnham aliunda baraza lake jipya la mawaziri, akimteua Waziri wa zamani wa Ulinzi John Healey kuwa waziri wa fedha, kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Healey alijiuzulu nafasi ya waziri wa ulinzi mwezi uliopita kufuatia kutokukubaliana juu ya mipango ya matumizi ya ulinzi ya serikali iliyopita. Vyombo vya habari vya Uingereza vimeuelezea uteuzi wake huo kuwa hatua isiyotarajiwa.

Keir Starmer akitoa hotuba ya kuaga nje ya Mtaa No. 10 wa Downing jijini London, Uingereza, Julai 20, 2026. (Xinhua/Li Ying)
Chama cha Labour kilipoteza kwa kiasi kikubwa katika uchaguzi wa mitaa mwezi Mei, na kusababisha miito iliyozidi kuongezeka ndani ya chama ikimtaka Starmer kujiuzulu. Starmer alitangaza Juni 22 kwamba atajiuzulu kuwa kiongozi wa Labour na kuacha nafasi ya waziri mkuu mara tu mbadala wake atakapochaguliwa.
Sasa baraza jipya hilo la mawaziri la Burnham linapaswa kukabiliana na changamoto ambazo Starmer alishindwa kuzishinda, zikiwemo za ukuaji dhaifu wa uchumi, huduma za umma zilizo chini ya shinikizo, gharama kubwa za maisha na mazingira ya kisiasa yanayozidi kuwa ya mgawanyiko.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



