Mkoa wa Hainan Kusini mwa China wapanga kupiga marufuku mauzo ya magari yanayotumia nishati ya mafuta ifikapo 2030

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 15, 2026

Magari yanayotumia nishati mpya yakionekana kwenye eneo la kielelezo la kaboni-sifuri la Boao, Mkoa wa Hainan, kusini mwa China, Machi 26, 2026. (Xinhua/Wang Yiliang)

Magari yanayotumia nishati mpya yakionekana kwenye eneo la kielelezo la kaboni-sifuri la Boao, Mkoa wa Hainan, kusini mwa China, Machi 26, 2026. (Xinhua/Wang Yiliang)

HAIKOU - Mkoa wa kisiwa wa Hainan Kusini mwa China umeweka lengo la kupiga marufuku uuzaji wa magari ya injini za mwako ifikapo mwaka 2030, ukiongoza mpito wa nchi hiyo kuelekea magari yanayotumia nishati mpya (NEVs).

Ifikapo mwaka 2030, magari yote mapya yatakayoongezwa na yale yatakayochukua nafasi ya yaliyopo, iwe ya binafsi, ya huduma za umma au ya kibiashara katika mkoa huo wa Hainan, lazima yawe NEVs, isipokuwa magari ya matumizi maalum, kwa mujibu wa mpango wa mkoa huo wa 2026-2030 kwa kujenga eneo la kitaifa la kielelezo kwa ustaarabu wa ikolojia.

Inakadiriwa kwamba kufikia wakati huo, uwiano wa NEV katika jumla ya magari ya mkoa huo utaongezeka kutoka asilimia 23.75 mwaka 2025 hadi asilimia 45. Mkoa huo pia utaboresha mtandao wake wa miundombinu ya kuchaji, huku uwiano wa magari-kwa-vifaa-vya-kuchaji ukiwekwa chini ya 2.5 kwa 1, umesema mpango huo uliotolewa hivi karibuni.

Mkoa wa Hainan mwaka 2018 ulipendekeza kwa mara ya kwanza lengo la kupiga marufuku uuzaji wa magari yanayotumia mafuta ifikapo 2030, na kuwa eneo la kwanza la ngazi ya mkoa la China kutangaza lengo kama hilo. Mpango huo wa sasa unasisitiza kwamba mkoa huo unaendelea kwa hatu madhubuti katika kutekeleza lengo hilo.

Mpango huo umezua mijadala mtandaoni kwa kuwa uthibitisho wa hivi punde zaidi wa dhamira ya China katika kupunguza kaboni na kutumia NEVs wakati huu ambapo baadhi ya nchi za Magharibi zimerudi nyuma kwenye sera za kijani. Mwishoni mwa mwaka jana, Kamisheni ya Ulaya ilitangaza mipango ya kulegeza marufuku yake ya kivitendo kwa magari mapya ya injini za mwako kuanzia 2035, ikiashiria hatua kubwa ya kurudi nyuma.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya China, uzalishaji wa NEV ulifikia magari zaidi ya milioni 16.52 nchini China mwaka jana, na kuashiria ongezeko la asilimia 25.1 kutoka mwaka uliopita. Ofisi hiyo ilisema, hadi kufikia mwisho wa 2025, idadi ya NEV zinazotumika nchini humo ilikuwa imefikia milioni 43.97, ongezeko la milioni 12.57 kutoka takwimu za mwaka 2024.

Hadi kufikia Oktoba 2025, kiwango cha upenyaji wa NEV katika mkoa wa Hainan kilikuwa kimefikia asilimia 67.14, ikimaanisha kwamba magari mawili kati ya matatu yaliyosajiliwa hivi karibuni katika mkoa huo yalikuwa NEV. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, mkoa huo umeshika nafasi ya kwanza na ya pili kitaifa, mtawalia, kwa upande wa upenyaji wa NEV sokoni na sehemu ya NEV kwa umiliki wa jumla wa magari, idara ya viwanda na teknolojia ya kupashana habari ya Hainan imesema.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha