Lugha Nyingine
Watu 16 wafariki kwenye ajali ya basi katika Jimbo la Western Cape, Afrika Kusini
CAPE TOWN - Watu kumi na sita wamefariki dunia baada ya basi kupinduka kwenye barabara kuu ya N1 karibu na Touwsrivier, ambayo pia inajulikana kwa jina la Mto Touws, katika Jimbo la Western Cape nchini Afrika Kusini mapema jana Alhamisi, mamlaka za serikali za mitaa zimesema.
"Tunathibitisha tukio kwenye barabara kuu ya N1 karibu na Touwsrivier majira ya saa 6:40 usiku wa leo (Alhamisi), ambapo basi lililokuwa likisafirisha wakazi wa Afrika Kusini limepinduka," imesema Idara ya Usafiri ya Western Cape katika taarifa.
"Kwa huzuni kubwa, watu 16 wamepoteza maisha, wakati huohuo wengine wawili wamepata majeraha makubwa," imesema.
"Huduma za dharura zinaendelea kubaki eneo la tukio, zikitoa msaada na kusimamia tukio hilo," idara imesema, ikiongeza kuwa mfumo wa kusimamisha na kuruhusu magari kuondoka uliwekwa huku shughuli za uokoaji na urejeshaji zikiendelea.
Katika taarifa nyingine, Shirika la Usimamizi wa Trafiki Barabarani (RTMC), shirika la serikali lenye jukumu la kusimamia usalama barabarani nchini Afrika Kusini, limesema basi hilo lilikuwa likisafiri kutoka Cape Town kwenda Idutywa katika Jimbo la Eastern Cape.
Kwa mujibu wa RTMC, basi hilo linadaiwa kuhusika katika ajali ya gari moja baada ya dereva kulikwepesha ili kuepuka kugongana na gari la kubeba mizigo, kupoteza udhibiti na basi kupinduka.
"Ajali hiyo imesababisha vifo 16, abiria 20 wamepata majeraha na wamesafirishwa hadi Hospitali ya Worcester. Abiria 43 wamekataa matibabu," imesema RTMC.
Chanzo cha ajali hiyo bado kinachunguzwa na RTMC na Huduma ya Polisi ya Afrika Kusini.
Wakati huo huo, Wizara ya Uchukuzi ya Afrika Kusini imesema katika taarifa kwamba Waziri wa Uchukuzi wa Afrika Kusini Barbara Creecy na Naibu Waziri Mkhuleko Hlengwa wametoa rambirambi kwa familia za waathiriwa na kuwatakia waliojeruhiwa ahueni ya haraka.
Wizara hiyo imesema mawaziri pia wameagiza Mfuko wa Ajali za Barabarani (RAF) kutoa usaidizi kwa familia zilizofiwa na abiria waliojeruhiwa.
Imeongeza kuwa RTMC imeagizwa kuchunguza chanzo cha ajali hiyo kwa ushirikiano na mamlaka za serikali za mitaa, huku ripoti ya awali ikitarajiwa ndani ya saa 48 mara tu uchunguzi utakapoanza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



