Lugha Nyingine
Botswana na Rwanda zaapa kuimarisha uhusiano

Rais wa Botswana Duma Boko (kulia) akisalimiana na Rais wa Rwanda Paul Kagame, Gaborone, Botswana, Mei 6, 2026. (Picha na Tshekiso Tebalo/Xinhua)
GABORONE - Botswana na Rwanda zimesisitiza dhamira zao katika kuzidisha uhusiano, kufuatia kusainiwa kwa makubaliano sita ya pande mbili Jumatano wiki hii mjini Gaborone, mji mkuu wa Botswana.
Rais wa Rwanda Paul Kagame alianza ziara ya kiserikali ya siku mbili nchini Botswana mapema Jumatano. Rais wa Botswana Duma Boko ameielezea ziara hiyo kuwa ya upangaji upya wa kimkakati unaolenga kubadilisha maono ya pamoja kuwa hatua halisi ndani ya muda mahsusi uliopangwa.
Makubaliano hayo yanahusu kuepuka kutozana kodi mara mbili, msamaha wa visa, afya, na biashara na uwekezaji wa kiuchumi.
Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari Jumatano, Rais Boko amesifu "uhusiano wa kidugu na wa kirafiki" kati ya mataifa hayo mawili na kutoa wito wa hatua za haraka kutekeleza makubaliano hayo.
"Tuko katika mbio dhidi ya wakati," amesema.
Boko ameorodhesha elimu, afya, kilimo, uwezeshaji wa vijana, michezo, ajira, miundombinu, na muunganisho wa kikanda kuwa ni maeneo ya kipaumbele kwa ajili ya ushirikiano.
Kwa upande wake Rais Kagame amesifu uhusiano wa pande mbili kuwa ni ushirikiano ulijengwa kwenye msingi wa malengo ya pamoja, akitolea mfano uboreshaji wa muunganisho wa anga, uwezeshaji wa visa, na makubaliano ya kuepuka kutozana kodi mara mbili kuwa ni hatua za kuondoa vizuizi vya uwekezaji.
Amesifu usimamizi wenye busara wa Botswana wa maliasili, hasa almasi, kwa ajili ya manufaa ya watu wake.
Rais Kagame amesifu uwekezaji wa Botswana katika uwezo wa dawa na uhimilivu wa usalama wa afya kuwa ni michango kuelekea kujitegemea kwa bara.
Amesema kuwa ushirikiano unapanuka zaidi ya haki na usalama hadi kuingia kwenye biashara, huku ushiriki hai wa jumuiya ya wafanyabiashara wakati wa ziara hiyo ukiashiria fursa halisi.
"Tunachokubaliana hapa lazima kibadilishwe kuwa maboresho halisi katika maisha ya raia wetu," Rais Kagame amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



