Benin yafanya uchaguzi wa amani wa rais huku idadi ya wanaopiga kura ikiwa ya chini zaidi kuliko ilivyotarajiwa

(Tovuti ya Gazeti la Umma) April 13, 2026

Mpiga kura akipiga kura yake kwenye kituo cha kupigia kura mjini Cotonou, Benin, Aprili 12, 2026. (Picha na Seraphin Zounyekpe/Xinhua)

Mpiga kura akipiga kura yake kwenye kituo cha kupigia kura mjini Cotonou, Benin, Aprili 12, 2026. (Picha na Seraphin Zounyekpe/Xinhua)

COTONOU - Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa 1:00 asubuhi kwa saa za Cotonou (06:00 GMT) jana Jumapili kote nchini Benin kwa ajili ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais, ambapo wapiga kura wanachagua rais atakayechukua nafasi ya Rais wa sasa Patrice Talon, ambaye muda wake wa kushika madaraka utaisha Mei 23.

Wafanyakazi wa uchaguzi walianza kuandaa mahitaji yote ya lazima mapema saa 12:00 asubuhi huko Cotonou, mji mkuu wa kiuchumi wa nchi hiyo, vilevile katika maeneo ya karibu, yakiwemo ya Godomey, Abomey-Calavi na Akassato. Maofisa kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Benin (CENA) wamesema kupelekwa kwa mahitaji yote ya lazima kwa kupigia kura kwa wakati kumehakikisha kwamba vituo vya kupigia kura vinafunguliwa kama ilivyokuwa imepangwa.

"Tayari tulikuwa na mahitaji ya lazima kwa kupigia kura kwenye kituo, na asubuhi ya leo tumepokea kura za karatasi na masanduku ya kupigia kura. Hii imetuwezesha kufungua vituo vya kupigia kura kwa wakati," Firmin Assogba, mkuu wa kituo cha kupigia kura cha Cadjehoun mjini Cotonou, ameliambia Shirika la Habari la China, Xinhua.

Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, rais na makamu wa rais wa nchi hiyo wanachaguliwa na wananchi wote kwa kupigia kura moja kwa moja, na muda wao wa kushika madaraka ni wa miaka saba.

Wagombea wawili wawili wanagombea uchaguzi huo: Waziri wa Fedha wa Benin Romuald Wadagni na mgombea mwenza wake Mariam Chabi Talata wa muungano tawala, na Paul Hounkpe na Rock Hounwanou wa chama cha upinzani cha Cowry Forces kwa Benin Inayoibuka.

Kama hakuna mgombea atakayepata kura nyingi za kuamua mshindi moja kwa moja katika duru ya kwanza, duru ya pili itafanyika Mei 10.

Kwenye vituo vya kupigia kura vilivyotembelewa na mwandishi wa habari wa Xinhua mjini Cotonou na maeneo ya jirani, shughuli za kupiga kura ziliripotiwa kuendelea vizuri na kwa amani.

"Habari zilizotolewa kutoka vituo vya kupigia kura kote nchini zimesema, shughuli za kupiga kura zilianza vizuri kwa wakati," amesema Armand Bognon, mjumbe wa jukwaa la asasi za kiraia lililotuma waangalizi 1,721 kote nchini, wakiwemo 1,200 walio kwenye vituo visivyohamishika na 521 kwenye vituo vinavyohamishika.

Ingawa hali ya utaratibu wa kupigia kura ni nzuri, idadi ya wapiga kura ilibaki kuwa ya chini wakati wa asubuhi na karibu adhuhuri, huku raia wakifika polepole kupiga kura zao. Kwenye vituo vingi vya kupigia kura, mahudhurio yalielezewa kuwa ya wastani, na baadhi ya wapiga kura walikwenda kwanza ibada za kidini za Jumapili kabla ya kuelekea kupiga kura.

"Zimebaki saa tatu kabla ya sisi kufunga kituo chetu cha kupigia kura saa 10:00 jioni. Lakini hali inayotushangaza ni kwamba, bado hatujaona idadi inayotarajiwa ya watu waliopiga kura. Wapiga kura wanawasili wachache wachache kwa kutimiza wajibu wao wa kiraia, ingawa wakati wa ibada za kanisani zilikuwa tayari zimeisha kabla ya saa sita mchana," mfanyakazi wa kituo cha kupigia kura katika eneo la Zoundja, wilaya ya Abomey-Calavi, ameliambia shirika la habrai la Xinhua kwa kuomba kutotajwa jina.

Kwa mujibu wa CENA, wapiga kura wapatao milioni 7.9 waliojiandikisha kupiga kura walikuwa wakitarajiwa kupiga kura kwenye vituo 17,562 vya kupigia kura kote nchini humo, huku matokeo ya awali yakitarajiwa kutangazwa ndani ya saa 48 baada ya kumalizika kwa zoezi la kupiga kura.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha