Wang Yi asema kutotumia nguvu ya jeshi au tishio la kijeshi kunasaidia pande zote, ikiwemo Israeli

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 04, 2026

BEIJING - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema kujiepusha na matumizi ya nguvu ya kijeshi au tishio la kutumia nguvu ya kijeshi katika mahusiano ya kimataifa ni kwa maslahi ya msingi ya pande zote, ikiwemo Israeli.

Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ametoa kauli hiyo jana Jumanne alipofanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israeli Gideon Sa'ar.

Baada ya kusikiliza maelezo ya Sa'ar juu ya msimamo wa Israeli kuhusu hali ya sasa, Wang amesema kwamba China bila kuyumbayumba imekuwa ikitetea kutatua masuala ya kimataifa na ya kikanda kupitia mazungumzo na mashauriano, na kwamba pande zote zinapaswa kufuata madhumuni na kanuni za Katiba ya Umoja wa Mataifa.

“Kwa miaka mingi, China imekuwa ikijitolea kuhimiza suluhu ya kisiasa ya suala la nyuklia la Iran,” Wang amesema, akiongeza kuwa mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Iran na Marekani yalikuwa yakipiga hatua dhahiri na pia kushughulikia wasiwasi wa usalama wa Israeli.

“Kwa masikitiko, mchakato huu sasa umevurugwa na mashambulizi ya kijeshi,” Wang amesema.

“China inapinga mashambulizi ya kijeshi yaliyoanzishwa na Israeli na Marekani dhidi ya Iran. Matumizi ya nguvu kiukweli hayawezi kutatua suala hilo. Badala yake, yataleta matatizo mapya na matokeo mabaya,” Wang amesema.

“Thamani ya kweli ya nguvu za kijeshi haiko kwenye uwanja wa vita bali katika kuzuia vita,” amesema Wang, akibainisha kuwa China inatoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa opereseheni hizo za kijeshi ili kuzuia mgogoro huo kupamba moto zaidi na kuenea kufikia hatua isiyodhibitika.

Amesema kwamba China bila kuyumbayumba imekuwa ikishikilia msimamo wa haki juu ya masuala ya Mashariki ya Kati na itaendelea kubeba jukumu la kiujenzi katika kuhimiza kutuliza hali.

Wang pia ameuhimiza upande wa Israeli kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi na taasisi za China. Sa'ar amesema kwamba Israeli inaweka umuhimu mkubwa kwenye jambo hilo na italinda usalama wa wafanyakazi na taasisi za China.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha