Lugha Nyingine
Mashambulizi ya Israeli yapiga vitongoji vya Beirut na kusini mwa Lebanon, maelfu wakimbia makazi

Moshi ukifuka kwenda angani baada ya shambulizi la anga la Israeli kwenye tawi la Taasisi ya Al-Qard Al-Hassan yenye uhusiano na Hezbollah, Mashgharah, mashariki mwa Lebanon, Machi 2, 2026. (Picha na Taher Abu Hamdan/Xinhua)
BEIRUT/JERUSALEM - Jeshi la Israeli lilianzisha mashambulizi ya anga jana Jumatatu kwenye vitongoji vya kusini mwa Beirut na vijiji vya kusini mwa Lebanon, yakisababisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao, kituo cha televisheni cha Al Jadeed nchini humo kimeripoti.
Mashambulizi zaidi ya sita yamepiga kitongoji cha Dahieh cha Beirut, huku mengine zaidi yakitokea kusini. Mashambulizi hayo yamefuatia tahadhari ya kuwataka watu kuondoka iliyotolewa na msemaji wa Jeshi la Israel Avichay Adraee.
Video kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha uharibifu mkubwa katika kitongoji hicho cha Dahieh na miji kadhaa ya kusini.
Vyombo vya habari nchini humo vimesema mashambulizi hayo yalilenga matawi ya Al-Qard Al-Hassan, ambayo Israeli inayaelezea kuwa ni taasisi ya mambo ya fedha yenye uhusiano na Hezbollah, katika maeneo yakiwemo ya Nabatieh, Tyre, Ain Qana, na Toul. Kundi hilo hutoa mikopo isiyo na riba na huduma za kibenki kwa waungaji mkono wa vuguvugu hilo linaloungwa mkono na Iran.
Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha MTV cha Lebanon amesema watu takriban 25,200 wamekimbia makazi yao kutoka kusini na mashariki mwa Lebanon na vitongoji vya kusini mwa Beirut.
Mivutano imepamba moto baada ya Hezbollah kurusha roketi nchini Israeli, na kusababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi. Jeshi la Israeli limeonya kwamba litaendelea kulenga maeneo ya Al-Qard Al-Hassan na limewasihi wakazi walio karibu kuhama angalau mita 300, shirika la habari la serikali ya Lebanon limeripoti.
Jeshi la Israeli limesema lilipiga maeneo zaidi ya 70 nchini Lebanon katika kipindi cha siku iliyotangulia, likilenga maghala ya kuhifadhia silaha ya Hezbollah, maeneo ya kurushia roketi, na vifyatulia makombora baada ya mashambulizi hayo ya kuvuka mpaka.

Picha iliyopigwa Machi 2, 2026 ikionyesha matokeo ya shambulizi la anga la Israeli dhidi ya tawi la Taasisi ya Al-Qard Al-Hassan yenye uhusiano na Hezbollah, Mashgharah, mashariki mwa Lebanon. (Picha na Taher Abu Hamdan/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



