Lugha Nyingine
Trump asema mazungumzo na Iran yataendelea ili kuona kama makubaliano yanaweza kufikiwa
WASHINGTON - Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba mazungumzo kati ya Marekani na Iran yataendelea ili kuona kama makubaliano yanaweza kufikiwa, muda mfupi baada ya mkutano wake wa faragha na Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya White House, Washington, D.C jana Jumatano.
"Nimemaliza punde mkutano na Waziri Mkuu Netanyahu wa Israeli, na wawakilishi wake mbalimbali," Trump amesema katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social.
"Hakukuwa na makubaliano ya mwisho yalilyofikiwa zaidi ya kusisitiza kwamba mazungumzo na Iran yaendelee ili kuona kama makubaliano yanaweza kufikiwa au la. Kama yanaweza, nitamjulisha Waziri Mkuu kwamba hilo litakuwa chaguo bora. Kama hayataweza, tutalazimika tu kuona ni matokeo gani yatatokea." amesema, akiongeza kuwa viongozi hao wawili wamejadili maendeleo yaliyopatikana katika Ukanda wa Gaza na eneo hilo kwa ujumla.
Netanyahu aliwasili katika Ikulu ya White House kwa gari kupitia South Lawn Jumatano asubuhi na kuondoka bila kufanya mkutano na waandishi wa habari wala kutoa taarifa yoyote.
Mkutano huo ulikuwa wa saba tangu kuanza kwa muhula wa pili wa Trump, umeripotiwa kuchukua saa takriban tatu.
Kabla ya mkutano huo, Netanyahu alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na kusaini ushiriki wake kuwa mjumbe wa "Bodi ya Amani." Mpango huo una utata katika Bunge la Israeli, Kituo cha Habari cha Fox kimeripoti.
Kabla ya safari yake hiyo ya Washington, Netanyahu aliwaambia waandishi wa habari: "Nitawasilisha kwa rais dhana yetu kuhusu kanuni za mazungumzo (juu ya Iran) -- kanuni zinazohitajika ambazo ni muhimu si kwa Israeli pekee bali kwa yeyote anayetaka amani na usalama katika Mashariki ya Kati."
Ofisi ya Netanyahu imesema kwamba waziri mkuu huyo anataka mazungumzo hayo yajumuishe kuweka kikomo kwenye mpango wa makombora ya balistiki wa Iran na kukata uhusiano wa Iran na makundi ya wanamgambo kama vile Hamas na Hezbollah.
Trump alisema Jumanne kwenye mahojiano na Kipindi cha Fox Business kwamba "lazima yawe makubaliano mazuri. Hakuna silaha za nyuklia, hakuna makombora."
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema katika sherehe mjini Tehran za kuadhimisha miaka 47 tangu kufanyika Mapinduzi ya Kiislamu ya 1979 Jumatano kwamba "ukuta wa kutoaminiana" uliojengwa na nchi za Magharibi unazuia mazungumzo ya nyuklia na Marekani, akiapa kwamba Iran haitasalimu amri kwa madai na uchokozi uliokithiri.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



