AU yalaani shambulio lililosababisha vifo katikati mwa Nigeria

(CRI Online) Februari 06, 2026

Umoja wa Afrika (AU) Jumatano ulilaani shambulio la kigaidi lililosababisha vifo katika Jimbo la Kwara lililopo katikati mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini humo, watu wasiojulikana wenye silaha walishambulia vijiji viwili katika Jimbo la Kwara Jumanne jioni na kurudi tena mapema Jumatano. Imeripotiwa kwamba, idadi ya vifo imeongezeka hadi kufikia zaidi ya 100 kufikia Jumatano mchana wiki hii baada ya watu hao wenye silaha kuanzisha shambulio la pili.

AU imesema katika taarifa yake kwamba Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU Mahmoud Ali Youssouf ameshtushwa na shambulio hilo ambalo limesababisha raia takriban 162 wasio na hatia kupoteza maisha yao kikatili.

Youssouf amelielezea shambulio hilo kuwa ni "kitendo kibaya na cha kikatili, ambacho kinakiuka sana haki za binadamu na ni shambulio lisilokubalika dhidi ya amani na usalama".

Aidha ameeleza mshikamano kamili wa AU kwa serikali na watu wa Nigeria katika wakati huu mgumu, akisisitiza dhamira ya AU kuendelea kuiunga mkono Nigeria katika juhudi zake za kuimarisha amani, usalama, na utulivu kote nchini.

(Wahariri wa tovuti:Zhao Jian)

Picha