Wagonjwa wa Palestina waanza kuondoka Khan Younis kuelekea mpaka wa Rafah ili kuvuka

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 03, 2026

Wagonjwa wa Palestina na watu wanaoambatana nao wakisubiri nje ya jengo la Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina, mjini Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, wakijiandaa kuvuka kupitia kivuko cha mpakani cha Rafah kwa ajili ya matibabu, Februari 2, 2026. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

Wagonjwa wa Palestina na watu wanaoambatana nao wakisubiri nje ya jengo la Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina, mjini Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, wakijiandaa kuvuka kupitia kivuko cha mpakani cha Rafah kwa ajili ya matibabu, Februari 2, 2026. (Picha na Rizek Abdeljawad/Xinhua)

GAZA - Vyanzo vya habari kutoka huduma za matibabu za Palestina vimesema jana Jumatatu kuwa baadhi ya wagonjwa wa Palestina wameanza kuondoka Khan Younis kuelekea kivuko cha Rafah kusini mwa Gaza, katika maandalizi ya kusafiri kwenda nje ya nchi.

Vyanzo hivyo vya habari vimeliambia Shirika la Habari la China, Xinhua kwamba basi la kwanza, lililobeba wagonjwa watano na watu 10 wanaoambatana nao, liliondoka kutoka makao makuu ya Shirika la Hilali Nyekundu la Palestina mjini Khan Younis na kuelekea kivuko cha Rafah kwenye mpaka wa Misri.

Atef al-Hout, Mkurugenzi wa Kituo cha Matibabu cha Nasser mjini Khan Younis, amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba upande wa Israeli umeidhinisha majina matano pekee kutoka kwenye orodha ya wagonjwa na watu 27 waliojeruhiwa, akibainisha kuwa suala la usafiri wao bado limegubikwa na "utata na ukosefu wa uwazi."

Mapema siku hiyo ya Jumatatu, kivuko hicho, ambacho ni njia pekee inayounganisha Gaza na Misri, kilifunguliwa tena pande zote mbili kwa kiwango kidogo na kwa majaribio, huku Wapalestina kadhaa wakiwasili upande wa Misri wa kivuko hicho wakijiandaa kuingia Gaza, kwa mujibu wa vyanzo vya Palestina.

Kivuko hicho, ambacho hapo awali kilikuwa njia kuu ya kutokea kwa Wapalestina na lango muhimu la kuingizia misaada ya kibinadamu, kimekuwa kimefungwa kwa kiasi kikubwa tangu Mei 2024, wakati vikosi vya Israeli vilipochukua udhibiti wa upande wa Palestina wa kivuko hicho. Kufunguliwa tena kwake kunaashiria hatua muhimu kufuatia makubaliano ya hivi karibuni ya kusimamisha mapigano kati ya Israel na Hamas,yaliyotangazwa kuanza kutekelezwa Oktoba 10, 2025.

Katika habari nyingine, Wapalestina watatu, akiwemo mtoto, wameuawa jana Jumatatu kwa mashambulizi ya jeshi la Israeli katika maeneo mbalimbali ya Gaza, kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya Palestina.

Vyanzo vya habari kwenye Kituo cha Matibabu cha Nasser vimesema mtoto mwenye umri wa miaka 3, Iyad al-Rabai'a ameuawa wakati manowari za Jeshi la majini la Israeli ziliposhambulia mahema yaliyokuwa yakihifadhi watu waliokimbia makazi yao kusini mwa Khan Younis.

Kituo hicho pia kilipokea mwili wa mwanamume mwenye umri wa miaka 40 aliyeuawa kwa mashambulizi ya jeshi la Israeli katika eneo la Khan Younis, vyanzo hivyo vimesema.

Hakukuwa na kauli ya mara moja kutoka upande wa Israeli kuhusu matukio hayo.

Tangu makubaliano ya hivi karibuni ya kusimamisha mapigano kuanza kutekelezwa, angalau Wapalestina 526 wameuawa kwa mashambulizi ya Israeli, na kufanya jumla ya vifo tangu Oktoba 2023 hadi kufikia 71,800, mamlaka za afya za Gaza zimesema jana Jumatatu.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha